Mwambe awacharukia wamiliki wa viwanda Tanzania
Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe ametoa onyo kali kwa wawekezaji wa viwanda nchini wanaowabagua na kutokuwatumia kikamilifu wataalamu wa ndani ya nchi katika shughuli zao
- Ni wale wanaowadharau na kuwabagua wataalam wazawa.
- Amewataka kuwarithisha ujuzi ili waendeleze viwanda.
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe ametoa onyo kali kwa wawekezaji wa viwanda nchini wanaowabagua na kutokuwatumia kikamilifu wataalamu wa ndani ya nchi katika shughuli zao, jambo linalowazuia kupata ujuzi unaohitajika katika maendeleo ya viwanda.
Waziri Mwambe ametoa onyo hilo leo Machi 17, 2021baada ya kuambatana na kamati ya kudumu ya bunge ya Viawanda, Biasharana Mazingira kutembelea kiwanda cha kutengeneza nyaya za umeme, transfoma na nguzo za zege cha Everwell Cable & Engineering kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
“Mahusiano na imani ya wenye kiwanda kuhusu wataalam wa ndani, hawaamini wataalamu wa ndani na nafasi zao zipo chache na wanaamini watu wao kutoka nje ndiyo wanafaa sana, hicho kitu kimenikela sana hata kamati hajapendezwa na hicho kitu,” amesema Mwambe.
Akiwa kiwandani hapo ameshuhudia kutengwa kwa Watanzania katika eneo la chakula na maeneo ya kufanyia kazi, jambo linaloashiria kuna ubaguzi katika utendaji wa kazi.
Baada ya kuona hali hiyo ameagiza uongozi wa kiwanda hicho kutengeneze umoja wa watumishi ili kuondoa dhana ya matabaka.
Aidha, Waziri Mwambe ametoa wito kwa wawekezaji wote kuweka mpango wa kuwafundisha wataalam wa ndani na kuwajengea uwezo ili kuepuka kuwatumia wataalam wa nje.