November 24, 2024

Ugonjwa wa figo bado tishio Tanzania

Njia za kujihadhari na ugonjwa huo zimetajwa zikiwa ni pamoja na kupunguza ulaji wa nyama na mayai kwa wingi.

  • Watanzania zaidi ya 5,000 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa sugu wa figo.
  • Njia za kujihadhari na ugonjwa huo zimetajwa zikiwa ni pamoja na kupunguza ulaji wa nyama na mayai kwa wingi.

Dar es Salaam. Taarifa za mtu kugundulika kuwa ana ugonjwa wa figo, huwa haziwafurahishi kabisa wanafamilia kwa sababu humbatana na gharama kubwa za matibabu ambazo zinaweza kuitumbukiza familia kwenye umaskini.

Mgonjwa naye huanza safari ya maisha mapya ya kubadili mtindo wa maisha ikiwemo kuanza kula baadhi ya vyakula ili kujiweka salama.

Machi 11, 2021 ilikuwa Siku ya Figo Duniani ambapo wadau mbalimbali wa afya wamezungumzia juu ya afya ya figo na nini kinatakiwa kuzingatiwa na mtu ili kuwa na figo zenye afya.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto, kupitia ukurasa wa Instagram (@elimu_ya_Afya) ugonjwa wa figo unaweza kuzuilika kwa kunywa maji walau glasi sita hadi nane kwa siku, kupunguza kula vyakula vilivyo na chumvi nyingi pamoja na kupunguza kula nyama na mayai.

Licha ya elimu hiyo kutolewa, bado haibadilishi hali ya watu ambao tayari wamepata maradhi hayo na wanapambana kujinasua katika ugonjwa huo ambao unaitesa dunia kwa sasa. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima akizungumza katika tamko maadhimisho ya Siku ya Figo Machi 11 alisema zaidi ya Watanzania 5,000 wanakadiriwa kuwa wagonjwa sugu wa figo hivyo kuwashauri Watanzania kuzingatia kanuni nzuri za afya ili kuwa salama.