Netflix kuwavalia njuga wasiolipia akaunti zao
Mtumiaji atatakiwa kuthibitisha akaunti yake kwa njia ya anuani ya barua pepe ambapo atatumiwa neno siri la kuthibitisha.
- Imesema ni kwa sababu za kibiashara na kiusalama.
- Mtumiaji atatakiwa kuthibitisha akaunti yake kwa njia ya anuani ya barua pepe ambapo atatumiwa neno siri la kuthibitisha.
Dar es Salaam. Kampuni inayosimamia programu tumishi ya simu (App) ya Netflix ya kutazama filamu imeanza kufanya majaribio ya kudhibiti watu wanaotumia akaunti za app hiyo bila kuzilipia.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la The Verge, udhibiti huo utaanza kwa kila mtumiaji wa akaunti ya Netflix kuthibitisha akaunti yake kwa kuiunganisha na anuani ya baruapepe ambayo imesajili akaunti yake.
Netflix yenye watumiaji zaidi ya milioni 200 imefikia maazimio hayo kwa sababu za kibiashara na kuisalama ili kulinda mapato na taarifa za watumiaji wake zisidukuliwe na watu wenye nia mbaya.
Soma zaidi:
- Coming to America: Filamu maalum kwa watu wasiotaka kuvunja viapo
- Serikali kuanzisha utalii wa meli Ziwa Victoria
- Maarifa wanayohitaji wafanyabiashara wadogo kustawisha biashara zao
“Endapo mtu atagundulika kuwa anatumia app hiyo bila uhalali, atalazimika kuthibitisha akaunti yake kwa njia ya baruapepe. Neno siri litatumwa katika barua pepe iliyosajilia akaunti hiyo na atalazimika kulithibitisha ndani ya muda fulani.
Tofauti na hapo, hatoweza kutumia huduma za Netflix,” imeeleza taarifa ya The Verge kuhusu hatua za Netflix.
Hatua hiyo ni muhimu katika kulifanya jukwaa hilo la filamu za mtandaoni kuwa salama kwa watumiaji wake. Lakini Netflix itakuwa na kibarua kigumu cha kudhibiti matumizi ya neno siri kwa watu zaidi ya mmoja hasa marafiki.
Pia Netflix inatakiwa kuzingatia kuwa, wapo watu ambao wamelipia akaunti zao na zinatumiwa na zaidi ya mtu mmoja zikiwemo familia, hivyo inaweza kuwa usumbufu ikiwa kila kifaa kinachotumia akaunti husika kutakiwa kufanya uthibitisho.