November 24, 2024

Mikakati ya Serikali ya Tanzania kukuza kilimo cha chai

Imesema itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa miche bora ili zao la chai lilimwe kwenye maeneo mbalimbali Tanzania.

Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda (kushoto) akitazama mtambo unaotumika kumwagilia mashamba ya chai ya wakulima wadogo Lwangu Wilaya ya Njombe. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya. Picha|Wizara ya Kilimo.


  • Itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa miche bora.
  • Itatumia wataalam wake wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na taasisi za fedha kupata mitaji kuboresha kilimo hicho. 

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ili kukabiliana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa zao la chai nchini, wizara yake itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa miche bora ili zao la chai lilimwe kwenye maeneo mbalimbali Tanzania. 

Amesema Wizara ya Kilimo itahakikisha inatumia wataalam wake wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na taasisi za fedha kupata mitaji itakayowekezwa kwenye kujenga miundombinu muhimu ya umwagiliaji ili zao la chai ambalo linastawi kwenye wilaya zaidi ya 12 nchini lilimwe na kuvunwa mwaka mzima.

“Tutafuta fedha toka kwa wadau wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili tujenge miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa chai, hatua itakayohakikisha tunaongeza uzalishaji wa majani mabichi ya chai mwaka mzima  badala ya kutegemea mvua” amesema Prof Mkenda akiwa mkoani Njombe hivi karibuni. 

Waziri Mkenda amesema ili kukuza uzalishaji wa zao la chai, suala la kutumia teknolojia ya umwagiliaji na matumizi ya miche bora ni muhimu na kuwa litaongeza tija kwenye kilimo hicho.  


Soma zaidi: 


Aidha, Waziri huyo wa kilimo aliagiza bodi ya chai na taasisi utafiti wa zao la chai (TRIT) kuzalisha miche bora ya chai na kuigawa kwa wakulima ili wapanue mashamba mapya na kuziba mapengo kwenye mashamba ya zamani.

Kwa mujibu wa Bodi ya Chai Tanzania, uzalishaji wa majani mabichi ya chai kwa mwaka umefikia tani 32,000 kutoka kwa wakulima kwenye wilaya zote 12 zinazolima zao hilo nchini.

Mikakati hiyo iliyoanishwa Prof Mkenda ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao cha wadau wa zao la chai kilichofanyika mkoani Njombe Machi 10 mwaka huu ambaye aliagiza Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wadau wa kilimo hicho ili kujua namna ya kutatua kero.