November 24, 2024

Utafiti kutegua kitendawili cha wafanyabiashara kukwepa kodi Tanzania

Serikali imesema inakamilisha utafiti wa kubaini visababishi vya kiwango cha chini cha ulipaji kodi kwa wakati na hiari hasa kwa wafanyabiashara wadogo Tanzania.

  • Serikali inakamilisha utafiti kuhusu visababishi vya kiwango cha chini cha uhiari wa walipakodi kusajili biashara zao, ulipaji wa kodi.
  • Mawakala kuanza kusimamia mashine za kukusanyia mapato (EFD)na siyo TRA. 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kukusanya na  kutumia Sh36.3 trilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, imesema inakamilisha utafiti wa kubaini visababishi vya kiwango cha chini cha ulipaji kodi kwa wakati na hiari hasa kwa wafanyabiashara wadogo Tanzania. 

Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Philip Mpango aliyekuwa  akisoma mpango na ukomo wa bajeti ya mwaka 2021/22 Machi 11 bungeni mjini Dodoma amesema katika fedha hizo, Sh23 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida  sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.

Kati ya mapato yote yatakayokusanywa, ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh26 trilioni sawa na asilimia 71.8 ya bajeti yote. 

Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo (Sh2.9 trilioni), mikopo ya ndani (Sh5 trilioni) na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara itakuwa Sh2.4 trilioni.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, katika kuhakikisha Serikali inakusanya kwa ukamilifu mapato ya ndani, imesema inakamilisha utafiti utakaosaidia kubaini sababu zinawafanya wafanyabiashara kutolipa kodi na kutoa taarifa sahihi kuhusu biashara zao.

“Serikali inakamilisha utafiti kuhusu visababishi muhimu vya kiwango cha chini cha uhiari wa walipakodi kusajili biashara zao, ulipaji wa kodi kwa wakati na uwazi katika utoaji wa taarifa sahihi kuhusu biashara wanazofanya, hususan kwa wafanyabiashara wadogo,” amesema Dk Mpango katika hotuba yake. 

Utafiti huo unahusisha kuchunguza changamoto za kitaasisi, tabia sababishi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuongeza kasi ya ulipaji kodi nchini.

Aidha, Dk Mpango amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatekeleza mradi wa kurejesha jukumu kusimamia mashine za kukusanyia mapato (EFD) kwa mawakala  ili kuongeza ufanisi katika usambazaji wa mashine za EFD pamoja na utoaji wa huduma za kiufundi pindi mashine hizo zinapopata hitilafu. 

“Vile vile, Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa mapato na matumizi kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa mapato yatakayokidhi ugharamiaji wa mahitaji ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti endelevu,” amesema Dk Mpango.