September 29, 2024

Kongamano la urithi wa ukombozi wa Afrika kufanyika Tanzania

Litawakutanisha wadau mbalimbali wa bara hilo jijini Dar es Salaam ili kuenzi mchango wa Tanzania katika ukombozi wa bara hilo.

  • Litawakutanisha wadau mbalimbali wa bara hilo jijini Dar es Salaam ili kuenzi mchango wa Tanzania katika ukombozi wa bara hilo. 
  • Kongamano hilo linafanyika chini ya programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo ilizinduliwa mwaka 2011.
  • Serikali inaendelea kuandaa mitaala ya vitabu vya masomo ya historia ya Tanzania na Afrika. 

Dar es Salaam. Serikali  inakusudia kufanya kongamano kubwa la kutambua na kuenzi mchango wa historia ya Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika ambalo litawakutanisha wadau mbalimbali wa bara hilo jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia litafanyika Machi 28 mwaka huu, katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) mkoani hapa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema mchango wa Tanzania katika kulikomboa bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, kutokana na kuhusisha Watanzania kujitoa kwa uhai wao, mali, vitu na maarifa kwa ajili ya kuliweka bara hilo kuwa huru. 

“Mchango wa Tanzania katika kulikomboa bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, Watanzania tunapaswa kujivunia Utanzania wetu, nasisitiza haya kwa kuwa vijana wengi wa sasa bado hawajafahamu suala hili ya kuwa Tanzania wakati wa ukombozi ilikuwa kama Macca au Jelusalemu ya Afrika, mchango wetu umetambulika duniani kote,” amesema Bashungwa.

Amesema kutokana na mchango huo wa Tanzania kwa Afrika, Mwaka 1963 Umoja wa nchi za Afrika uliekeleza Tanzania kuwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika hadi nchi ya Afrika Kusini ilipopata Uhuru Mwaka 1994 mwaka ambao nchi zote za Afrika zilikombolewa.

“Kutokana na juhudi hizo mwaka 2011 Umoja wa Afrika uliridhia Tanzania kuanzisha makao makuu ya kulinda, kuhifadhi na kuenzi Urithi wa Ukombozi wa Afrika kupitia programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika  na kuzielekeza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kushirikiana na Tanzania katika kuratibu program hii ambayo makao makuu yake ni Jijini Dar es Salaam,” amesema.


Zinazohusiana:


Kongamano hilo la siku moja litajumuisha Wadau wa Ukombozi, wawakilishi wa baadhi ya nchi zilizosaidiwa na Tanzania katika kupigania uhuru wao pamoja na wadau wengine huku wito ukiwa ni kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika kongamano hilo.

Kongamano hilo linafanyika chini ya programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo ilizinduliwa mwaka 2011 ambapo inalenga kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Aidha, Serikali inaendelea kukamilisha mitaala ya vitabu vya masomo ya historia ya Tanzania, ambavyo pamoja na mambo mengine, vitajumuisha mkusanyiko wa historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika na kutoa ufahamu kwa wanafunzi wa jinsi Tanzania ilivyojitoa katika kupigania uhuru wa nchi zingine.