September 29, 2024

Mafuta yachangia kushusha mfumuko wa bei Tanzania

Umeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Februari 2021 kutoka asilimia 3.5 mwaka ulioishi Januari 2021.

  • Umeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Februari 2021 kutoka asilimia 3.5 mwaka ulioishi Januari 2021.
  • Umechagizwa zaidi na kupungua kwa baadhi ya bei za bidhaa zisizo za vyakula ikiwemo petroli.
  • Bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeongezeka hadi asilimia 3.6  kutoka asilimia 2.8 kama ilivyorekodiwa Februari 2020.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Februari 2021 kutoka asilimia 3.5 mwaka ulioishia Januari 2021 ikichagizwa zaidi na kupungua kwa baadhi ya bei za bidhaa zisizo za vyakula ikiwemo petroli. 

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Machi 8, 2021), imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa hasa zisizokuwa za vyakula ikilinganishwa na Februari mwaka huu.

Baadhi ya bidhaa zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mafuta ya taa ambayo yamepungua kwa asilimia 15.7, vifaa vya nyumbani kama pasi ya umeme kwa asilimia 4.7, vyombo vya ndani (asilimia 3.3), dizeli (asilimia 22.8) na petroli kwa asilimia 13.4. 


Zinazohusiana: 


Kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeongezeka hadi asilimia 3.6  kutoka asilimia 2.8 kama ilivyorekodiwa Februari 2020.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2021, kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula katika kipindi kilichoishia Februari 2021 ikilinganishwa na bei za mwezi Februari 2020,” inasomeka sehemu ya ripoti ya mfumuko wa bei ya NBS.