November 24, 2024

Bandari ya Kigoma yaipa tabasamu Serikali ya Tanzania

Maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari ya Kigoma yameanza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa shehena ya mizigo pamoja na mapato.

  • Yameanza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa shehena ya mizigo pamoja na mapato.
  • Imeipiku Bandari ya Mwanza ambayo ndiyo iliyokuwa ikiongoza kabla ya maboresho hayo. 
  • Amesema bado kuna maboresho zaidi yanaendelea katika bandari Kuu ya Kigoma.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusidedit Kakoko amesema maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari ya Kigoma yameanza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa shehena ya mizigo pamoja na mapato. 

Mahandisi Kakoko amesema shehena na mapato katika bandari hiyo yameongezeka kiasi cha kuipiku Bandari ya Mwanza ambayo ndiyo iliyokuwa ikiongoza kabla ya maboresho hayo miongoni mwa bandari zilizopo kwenye maziwa. 

Bandari ya Kigoma ambayo inahusisha bandari zote zilizopo katika Ziwa Tanganyika imeanza kufanyiwa maboresho kuanzia mwaka 2016/17 ikihusisha ujenzi wa magati,  ununuzi wa mitambo, ujenzi wa maghala na majengo ya abiria pamoja na ujenzi wa ofisi za kisasa za makao makuu ya bandari hiyo ambazo ziko katika hatua za mwisho kukamilika.

Maboresho hayo yalisukumwa na kasi kubwa ya ongezeko la mahitaji ikilinganishwa na miundombinu iliyokuwepo, amesema Mhandisi huyo Februari 5, 2021 alipotembelea bandari hiyo.


Kufahamu alichoongea Mhandisi Kakoko kuhusu mafanikio yaliyopatikana baada ya maboresho ya Bandari ya Kigoma iliyopo Ziwa Tanganyika, tazama video hii

                         


Bandari za Ziwa Tanganyika zimekuwa kiungo kikubwa cha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Congo DRC, Burundi na Zambia, biashara kubwa ikiwa ni usafirishaji wa mazao yanayozalishwa Tanzania.

“Pia bandari hizo pamoja na kuanza kazi kwa reli kumesaidia kupunguza bei za bidhaa ambazo husababishwa na gharama kubwa za usafirishaji,” imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na TPA mapema leo Machi 6, 2021. 


Zinazohusiana:


Amesema bado kuna maboresho zaidi yanaendelea katika bandari Kuu ya Kigoma yanahusisha ujenzi wa gati ya maboti ya Kibirizi, gati ya abiria na makasha na ujenzi wa bandari Kavu ya Katosho.

Matarijio ya kuongezeka zaidi kwa shehena na abiria ni makubwa kutokana na maboresho ya meli yanayotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) zikiwemo MV Mwongozo,  MV Liemba na MT Sangara.

Tanzania ina bandari kuu sita ambapo tatu kati ya hizo zinapatikana kwenye maziwa makuu ya Nyasa, Victoria na Tanganyika.