September 29, 2024

Mrithi wa Maalim Seif nafasi ya makamu wa rais atangazwa Zanzibar

Ni mwanachama wa ACT-Wazalendo na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17 mwaka huu.

  • Ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17 mwaka huu. 
  • Othman aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ataapishwa kesho Februari 2, 2021 Ikulu Zanzibar. 

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amemteua mwanachama wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17 mwaka huu. 

Othman aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ataapishwa kesho Februari 2, 2021 Ikulu Zanzibar. 

“Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk Hussein Mwinyi amemteua Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar,” imeeleza taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena Said iliyotolewa leo mchana. 

Kuteuliwa kwa Othman kumekuja baada ya kumalizika kwa kikao kilichowakutanisha vigogo wa ACT-Wazalendo chini ya kiongozi wake mkuu, Zitto Kabwe mwisho mwa wiki kilichofanyika jijini Dar es Salaam kujadili jina la mtu atakayerithi nafasi iliyoachwa na Maalim Seif. 

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na katika mabadiliko yaliyofanyika mwaka 2010,  inatoa siku 14 kumpata mtu mwingine atakayeziba nafasi ya makamu wa rais baada ya mtu aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kuondoka au kufariki dunia. 


Soma zaidi:


Othman ambaye kitaaluma ni mwanasheria anakumbkwa kwa kitendo cha kujiuzulua katika nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya mwaka 2014 iliyokuwa chini Bunge la Katiba lililokuwa linaongozwa na Hayati Samuel Sitta.

Othman alifikia hatua hiyo baada ya kupendekezwa mambo 17 yenye maslahi kwa Zanzibar yaingizwe ndani ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge, lakini yalikatiliwa.

Kujiuzulu kwa kigogo huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kulizua taharuki ndani ya Bunge la Katiba na nje kutokana na nafasi aliyokuwa nayo serikalini. 

Kutokana na sintofahamu hiyo, iliwalazimu viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Othman alikuwa mwanachama kuazimia kufukuzwa kazi kwa mwanasheria huyo kwa kile walichodai amekisaliti chama.