September 29, 2024

Tanzania kuongeza helikopta kutokomeza nzige wa jangwani

Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuongeza ndege ya pili katika mapambano ya kutokomeza nzige wa jangwani waliovamia baadhi maeneo ya wilaya za mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.

  • Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuongeza ndege ya pili katika mapambano ya kutokomeza nzige wa jangwani waliovamia baadhi maeneo ya wilaya za mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.
  • Waziri wa kilimo aeleza kuwa tathmini ya awali yaonyesha nzige hawajaathiri mashamba na malisho.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuongeza ndege ya pili katika mapambano ya kutokomeza nzige wa jangwani waliovamia baadhi maeneo ya wilaya za mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania mwishoni mwa Januari mwaka huu.

Hatua hiyo ni sehemu ya muendelezo wa mapambano dhidi ya wadudu hao waharibifu ambao hadi sasa wameripotiwa kuwepo katika halmashauri za Siha, Simanjiro na Longido.

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amewaambia wanahabari mjini Moshi mkoani Kilimanjaro leo Machi mosi 2021 kuwa hadi sasa wanaendelea kukabiliana na nzige hao kwa kutumia helkopta kutoka Shirika la Nzige Wekundu (RLCO).

“Serikali itaongeza ndege ya pili kutoka shirika la Nzige wa Jangwani (DLCO) kupulizia makundi madogo ya nzige walionekana maeneo ya Wilaya za Longido kufuatia uwepo wa taarifa kuwa nzige wachanga kutoka Kaunti ya Machakos nchini Kenya wanaweza ingia Longido,” amesema Prof Mkenda katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Waziri huyo, ambaye pamoja na naibu wake Hussein Bashe wamekuwa katika maeneo  yaliyovamiwa na nzige hao, amewaambia wanahabari kuwa hadi sasa wadudu hao wamedhibitiwa na wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana  na halmashauri za wilaya za Longido, Siha na Simanjiro.


Zinahusiana: 


Jitihada za kuangamiza makundi ya nzige waliosalia zinaendelea kwa kutumia helkopita na mabomba ya kupuliza kwa mikono, imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa wizara hiyo Revocatus Kassimba.

“Tupo makini kuwakabili nzige hadi sasa hatujapata madhara yoyote kwa mashamba ya wakulima hivyo Watanzania wasiwe na taharuki” amesema Prof Mkenda.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika Mashariki na pembe ya Afrika ambazo zimeguswa na uvamizi wa nzige wa jangwani ambao Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) linaeleza kuwa huenda ukaathiri mwenendo wa uzalishaji wa chakula na kupunguza usalama wa chakula katika ukanda huo.

Mei mwaka jana FAO ilisema kuwa hatua za wakati ule zilisaidia kuokoa tani 720,000 za nafaka na kunusuru kaya 350,000 za wafugaji.

FAO imeeleza katika ripoti yake ya wiki iliyopita kuwa makundi madogo ya nzige wadogo yanazidi kupungua Kaskazini na katikati mwa Kenya na kwamba hakukuwa na taarifa za Nzige wa Somalia kuingia nchini humo.

“Kulikuwa na makundi madogo ya nzige yaliyotokea kusini mwa Kenya na kuingia Kaskazini mwa Tanzania karibu na eneo la Mlima Kilimanjaro…katika wilaya za Longido na Kusini mwa mkoa wa Manyara,” inasomeka sehemu ya ripoti ya FAO kuhusu mwenendo wa nzige ya Februari 23, 2021.