Wabunge walalamikia miradi ya umeme vijijini kutokamilika Mwanza
Ni miradi inayosimamiwa na kampuni tanzu ya Shirika la umeme Tanzania ya ETDCO. Ilianza kutekelezwa mwaka 2018 katika vijiji 130 lakini mpaka sasa haijakamilika.
- Ni miradi inayosimamiwa na kampuni tanzu ya Shirika la umeme Tanzania ya ETDCO.
- Ilianza kutekelezwa mwaka 2018 katika vijiji 130 lakini mpaka sasa haijakamilika.
Mwanza. Wabunge wa Mkoa wa Mwanza wamesikitishwa na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya umeme vijiji katika mkoa huo licha ya kubadilishwa kwa mkandarasi anayesimamia miradi hiyo, jambo linalowakwamisha wananchi kufanya shughuli za maendeleo.
Kwa sasa miradi hiyo ya umeme iliyopo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika mkoa huo inatekeleza na kampuni tanzu ya Shirika la umeme Tanzania ya ETDCO ambapo awali ilikuwa inatekelezwa na kampuni ya Nipo Group.
Licha ya kubadilishwa mkandarasi, miradi hiyo imekuwa ikisuasua. Miradi hiyo ni pamoja na ule unaotekelezwa katika vijiji 130 vya mkoa huo ambao ulianza tangu 2018 chini ya NIPO Group na baadaye ikapewa ETDCO.
Kutokamilika kwa mradi huo kumewaibua wabunge wa mkoa wa Mwanza ambao licha ya kutaka majibu kutoka REA, pia wamedai kuwa huenda nguzo zilizomwagwa kwenye maeneo hayo kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana bado hazijafanyiwa kazi huku nyingine zilizokuwa zimesimikwa kuanza kuanguka.
Mbunge wa jimbo la Sumve, Mageni Kasalai amesema kabla ya kuanza kwa uchaguzi Mkuu nguzo nyingi zilimwagwa katika vijiji tofauti lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.
“Hiyo inawaondolea imani wananchi kuwa huenda nguzo hizo zilimwagwa kwa ajili ya kuwashawishi wapige kura kwa Chama Cha Mapinduzi kitendo ambacho si sahihi kwani hata zile walizozichimbia zimeanza kuanguka,” amesema Mageni.
Soma zaidi:
- Wadau wahimiza uwekezaji, uendelezaji nishati jadidifu Tanzania
- Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo
Naye Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor amesema changamoto nyingine inayowakumba Tanesco wilayani Kwimba ni ukosefu wa gari inayowasaidia kufika eneo la miradi kwa wakati.
“Tanesco Wilaya ya Kwimba haina gari, licha ya Waziri kuagiza gari linunuliwe toka mwaka juzi lakini hadi sasa hakuna utekelezaji hali inayochangia kushindwa kupeleka umeme majumbani,” amesema Mansoor.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula amesema ipo haja ya kumwalika Waziri wa Nishati pamoja na Mkurugenzi wa Rea kuhudhuria vikao hivyo ili kujibu changamoto zinazowakumba wajumbe hao.
“Vinginevyo tutakuwa tunatumia muda mrefu bila kupata majibu sahihi, hivyo nashauri katika vikao vijavyo viongozi hawa waalikwe wahudhurie vikao hivi ili kutupatia majibu sahihi,” amesema Mabula
Hata hivyo, malalamiko ya wabunge hayo yametolewa ikiwa ni miezi miwili tu toka Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani kuagiza kampuni tanzu ya ETDCO kuhakikisha inakabidhi mradi huo ndani ya siku 30.
Agizo la Waziri huyo lilitolewa mwishoni mwa mwezi Disemba wakati akizungumza na watumishi pamoja na watendaji wa Tanesco Mkoa wa Mwanza.