November 24, 2024

Serikali kuanzisha utalii wa meli Ziwa Victoria

Utasaidia kuzifikia hifadhi za Taifa katika ukanda huo kwa urahisi. Pia utasaidia kuongeza watalii wa nje ambao idadi yao imepungua.

  • Utasaidia kuzifikia hifadhi za Taifa katika ukanda  huo kwa urahisi.
  • Pia utasaidia kuongeza watalii wa nje ambao idadi yao imepungua. 

Dar es Salaam. Serikali imesema ina mpango wa  kuanzisha utalii wa meli katika Ziwa Victoria ili kufungua fursa za utalii katika hifadhi za Taifa zilizo karibu na ziwa hilo, jambo litakalosaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania. 

Utalii huo utahusisha watalii wote wa ndani na nje ya nchi ambao watakuwa wakitembelea hifadhali mbalimbali za Taifa ikiwemo  Serengeti,  kisiwa cha Rubondo,  Buligi na Saanane jijini Mwanza. 

Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii,  Marry Masanja amesema mpango huo umekuja baada ya kiwango cha watalii wanaotoka nje ya nchi kupungua kutokana na tatizo la ugonjwa wa corona lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2019 na hivyo kupunguza mapato yatokanayo na sekta hiyo. 

Kwa  mujibu  wa Naibu Waziri huyo anasema kabla ya ugonjwa huo idadi ya watalii waliokuwa wanaingia nchi mpaka mwishoni mwa Disemba 2019  walikuwa milioni 1.5.

“Takwimu zinabainisha kuwa toka mwaka 1993 sekta ya Utalii ilipokea watalii  230,000 idadi ambayo iliongezeka kila mwaka na kufikia 1.5 mwaka juzi ambao walifanya utalii katika mbuga mbalimbali za wanyama nchini, ” amesema Masanja katika kikao cha bodi ya barabara Jijini Mwanza leo Februari 25, 2020. 


 Zinazohusiana: 


Bila kutaja takwimu halisi, Naibu Waziri huyo amesema licha ya kuwepo kwa Corona, mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na idadi kubwa ya watalii walioingia nchini. 

“Licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa corona mwishoni mwa mwaka jana hoteli  zote za  kitalii zilijaa,” amesema Msanja huku akihimiza utalii wa ndani utakaosaidia kukabiliana na athari za janga hilo kwenye sekta ya utalii.

“Tulikuwa tukitegemea sana  watalii kutoka nje lakini kutokana na ugonjwa wa corona  walikwama kutokana na changamoto hiyo,  hivyo kama Watanzania hatuna budi kupenda  vya kwetu na kuvitangaza ili kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo, “amesema naibu waziri huyo.  

Alisema kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa kutangaza vivutio kwenye mitandao ya kijamii na kupokea watalii kutoka ndani na nje ya nchi, kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.