September 29, 2024

Vijana wageuza nywele za binadamu kuwa mbolea Tanzania

Ni vijana wa mkoani Arusha ambao wanatumia teknolojia ya aina yake ili kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira na ukosefu wa ajira kwa vijana.

  • Huzibadilisha nywele na kuwa mbolea na viuatilifu kwa ajili ya kilimo.
  • Teknolojia hiyo inasaidia kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira na ukosefu wa ajira kwa vijana.
  • Ndoto yao ni kujenga viwanda vingine vya urejelezaji wa nywele za binadamu Tanzania. 

Dar es Salaam. Huenda kwako na watu wengine, nywele za binadamu ambazo zimenyolewa ikawa ni uchafu unaopaswa kutupwa.

Hata hivyo, usichokijua ni kuwa kuzitupa nywele za kichwani au sehemu za siri, kunakukosesha fursa mbalimbali ambazo zingeweza kukutoa kimaisha.

Nywele zilizonyolewa siyo tu hutumika kutengeneza mawigi (natural wigs) bali ni malighafi muhimu ya uzalishaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ya kukuzia mimea. Huenda bado huamini kama inawezeka. 

Nchini Tanzania kuna vijana wabunifu ambao ndoto yao ni kuona taka zinazosambaa mitaani zinabadilishwa kuwa bidhaa inayoweza kutumiwa tena na binadamu. 

David Denis na wenzake wanaoishi mkoani Arusha wamekuwa vinara wa kurejeleza nywele za binadamu kuwa mbolea ya kukuzia mazao mbalimbali inayowafaa wakulima wadogo. 

David ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) anasema nywele za binadamu zina protini maalum ambayo ina virutubisho muhimu kwa ajili ya kukuzia mimea.

“Niligundua kwenye nywele pia kuna molekuli hizi za protini zinazoitwa “keratin”. Protini yoyote ina elementi ambazo pia ni virutubisho kwa mazao. Hivyo, wazo la kwanza lilikuwa kuzirejeleza nywele hizo za binadamu kuwa mbolea,” anasema kijana huyo ambaye mwaka jana alishinda tuzo ya Anzisha Prize inayowatambua vijana wabunifu wanaotatua matatizo ya jamii. 

Ugunduzi huo aliubaini wakati yuko kidato cha tano mwaka 2017 katika shule ya St. Jude ya jijini Arusha akiwa mwanafunzi anayesoma mchepuo wa Fizikia, Kemia na Biolojia ambapo darasani walifundishwa namna molekuli za kibaolojia kama protini zilivyo na zinavyofanya kazi.  

“Wazo la urejelezaji wa nywele hizi za binadamu lilitokana na uchafu wa nywele unaotoka kwenye saluni ya shule kila wiki unaoishia kuchomwa na kuongeza hatari kwenye afya ya wanafunzi na wafanyakazi,” David aliiambia Nukta (www.nukta.co.tz). 

David Denis akitoa somo jinsi wanavyorejeleza nywele za binadamu kuwa mbole mbele ya wanafunzi. Picha| David Denis. 

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kulifanya wazo hilo kivitendo yeye na marafiki zake akiwemo Ojung’u Jackson (ambaye sasa ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Botswana) baada ya kupata msaada kutoka kwa walimu.

Anasema baada ya kumaliza elimu ya sekondari, waliamua kuanzisha kampuni ya CuOff Recycle ambayo iko Arusha na kuajiri vijana 17 moja kwa moja kwenye kazi ya kuzichakata taka hizo kutengeneza mbolea kimiminika na viuatilifu vya kuua magugu shambani.

Ili kupata bidhaa hizo za shambani, nywele zilizokusanywa huchambuliwa vizuri na kuchanganywa kwenye kemikali maalum ili kupata kimiminika ambacho hutumika kama mbolea na viuatilifu. 


Uzalishaji, soko vinahitaji msuli zaidi

Hata hivyo, David anakiri kuwa bado uzalishaji siyo mkubwa kwa sababu, kampuni yake haina mtaji na teknolojia ya kisasa ambayo inarahisha mchakato wa utengenezaji bidhaa hizo.

“Kwa sasa urejelezaji unafanyika mdogo sana kutokana na kufanya hatua zote bila kuwa na mashine maalumu,” anasema David ambaye kampuni yake ilishinda tuzo ya Young Scientists Tanzania mwaka 2018 katika Wiki ya Ubunifu ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha kwa kushika nafasi ya pili. 

Teknolojia hiyo huusisha mashine tatu ambazo huchambua, hukausha na kuchanganya nywele pamoja na kemikali zingine. Mashine hizo zinaagizwa nje ya nchi na zote kwa pamoja zinagharimu takriban Sh200 milioni.

Kwa sasa, wanasambaza mbolea na viuatilifu hivyo kwa wakulima wadogo wadogo wa mboga za majani wa jijini Arusha ambapo lita moja ya mbolea wanauza kwa Sh1,000 na Sh1,500 kwa viuatilifu. 

“Hatuwezi kupanua soko letu kwa sasa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya tozo kubwa za kuidhinisha kila bidhaa tunayotengeneza. Lakini tuko mbioni ili kuweza kufikia soko kubwa la wakulima ambao wanauhitaji wa bidhaa zetu tayari,” anasema David ambaye ni mwanzilishi wa kampuni hiyo.  


Soma zaidi:


Malighafi siyo tatizo kwao

Licha ya kuwepo kwa changamoto ya teknolojia, upatikanaji wa malighafi ya nywele ni mkubwa kuliko hata kiwango wanachohitaji kwa sasa, jambo ambalo linawafanya wasugue vichwa kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo kuongeza uzalishaji ili kuwafikia wakulima wengi. 

“Upatikanaji wa malighafi yetu kuu (nywele za binadamu ambazo ni taka) si wa kutlia shaka kabisa. Saluni 70 tu tulizoweza kuzifikia hadi sasa Arusha zinatuzidi uwezo. Kwa wiki tuna uwezo wa kukusanya wastani wa kilo 500. Apo ni asilimia ndogo tu ya saluni zote Arusha,” anasema kijana huyo.

Kwa sasa, kampuni anayoingoza imeajiri watu zaidi ya 100 ambao wanakusanya taka za nywele za binadamu kutoka kwenye saluni na kuzichakata ili kupata bidhaa. 


Teknolojia hiyo inavyotunza mazingira

Nywele za binadamu zinazotupwa kwenye madampo ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira hasa vyanzo vya maji kwa sababu ya uwepo chembechembe hatarishi.

Urejelezaji wanaoufanya CutOff Recycle unasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuimarisha uchumi na kulinda afya za binadamu.

“Hata sisi tunafanya kazi kubwa ya kuepusha taka hizi kuongezeka kwenye dampo na kusababisha magonjwa ya milipuko kama kichocho lakini pia magonjwa ya mapafu. Nywele hizi pia huharibu vyanzo vya maji kutokana na kiasi kikubwa (17%) cha Nitrogen kilichonacho,” anaeleza David. 

Nywele za binadamu zikichambuliwa na kutenganishwa na taka zingine tayari kwa ajili ya kuchanganywa na kemikali ili kutengeneza mbolea. Picha| Cutoff Recycle. 

Kibarua alichanacho kijana huyo

Licha ya kazi nzuri anayofanya David kuokoa mazingira na kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo, bado ana kibarua kigumu cha kutafuta teknolojia na mtaji kurahisisha shughuli za urejelezaji wa taka za nywele.

Lakini pia kubadili mtazamo wa jamii kutokuamini kuwa nywele za binadamu zinaweza kutengeneza mbolea na viuatilifu kwa sababu wanazihusisha na ushirikina.

“Tanzania kama sehemu yeyote Afrika ina dhana hasi ya urejelezaji huu tunaofanya. Wanahusisha na uchawi. Nakumbuka wakati tunaanza hamna saluni ilikuwa tayari kutupa taka zao lakini walikua tayari kulipia kuwekwa kwenye gari la taka kila wiki,” anasema David.  

David ambaye amekuwa akitoa mafunzo ya teknolojia hiyo, anasema ana kazi kubwa ya kuelemisha jamii kuhusiana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia ambao unabadilisha na kuleta njia mpya za maisha kila siku.

“Changamoto kubwa ni kutokuwepo elimu ya kutosha kuhusu urejelezaji wa taka na hasa kama hizi tunazofanya sisi tunawachanganya watu kabisa sasa kibiashara inakwenda zaidi katika kuwataka wateja ambao ni wakulima waelewe kama inafanya kazi la sivyo watakuita mchawi,” anasema.  

Licha ya changamoto hizo, bado ana matarajio makubwa ya kuifanya kazi hiyo kuwa endelevu kwa kuanzishwa kiwanda kikubwa nchi Tanzania ambacho kitaajiri vijana wengi ili kusaidia kutunza mazingira na kuwarahisishia wakulima maisha.

Penye nia, kila kitu kinawezekana

“Mwaka ukiisha nataka watu zaidi ya 300 wengine wanufaike kutokana na mradi huu. Tutafungua kiwanda Dar es Salaam, halafu mikoa mingine tutaendelea mpaka tufikie miji yote mikubwa mwaka 2025,” anaeleza David.

“Nitoe tu hamasa, tunaweza tukifanya’” anaeleza David akiwataka vijana hasa ambao wako vyuoni kuweka jitihada mapema za kuboresha maisha yao kwa kuanza kujihusisha na vitu wanavyovipenda ili kuepuka changamoto za ukosefu wa ajira na kuongeza kuwa “Taifa letu litakuwa la watu wawajibikaji haya yakifanyika.”