November 24, 2024

Wajasiriamali vijana Tanzania kuwania kitita cha zaidi Sh230 milioni

Ni baada ya kuchaguliwa kuingia katika programu maalum ya mafunzo ya Anzisha Prize.

  • Ni baada ya kupata fursa ya kuingia katika programu maalum ya mafunzo ya  Anzisha Prize. 
  • Pia watakaoingia kwenye programu hiyo wajiweka katika nafasi ya kushinda tuzo ya Dola za Marekani 100,000 (Sh231.8 milioni). 

Dar es Salaam. Kama wewe ni kijana mjasiriamali hujui wapi utapata mtaji au maarifa ya kukuza biashara yako basi mlango umefunguliwa kwa ajili ya kutimiza ndoto zako.

Tuzo za Anzisha Prize zimefungua dirisha kwa wajasiriamali wakiwemo wa Tanzania kuomba kuingia katika programu maalum na kujiweka katika nafasi ya kushinda sehemu ya tuzo ya Dola za Marekani 100,000 sawa na Sh231.8 milioni.

Dirisha la programu hiyo inayojulikana kama Anzisha Prize limefunguliwa leo Februari 15, 2021 nchini Afrika Kusini na taasisi za Mastercard na African Leadership Academy ambapo wajasiriamali kutoka nchi za Afrika wako huru kutuma maombi yao ili kupata fursa hiyo adimu. 

Taarifa ya taasisi hizo mbili iliyotolewa leo inaeleza kuwa kutokana na janga la Corona kuharibu mifumo ya kibiashara duniani, vijana wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, hivyo kuna haja ya kuwasaidia ili walete mabadiliko endelevu.

“Namna dunia inavyofanya kazi baada ya kutokea kwa janga la Corona, vijana wajasiriamali wamebaki imara wakizisaidia jamii zao zinazopitia wakati mgumu. 

“Tuna kiu ya kuwasherekea vijana 20 wanaomiliki biashara, bila shaka watachangia kutengeneza ajira barani (Africa),” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Anzisha Prize, Melissa Mbazo-Ekpenyong.

Melisa amesema wajasiriamali watakaofadika na programu hiyo ni wenye umri wa miaka 15 na 22 ambao wanamiliki biashara na miradi ambayo inalenga kutatua matatizo ya kijamii na kuongeza ajira kwa wenzao.


Zinazohusiana: 


Watakaofanikiwa kuingia katika programu hiyo ambayo itaanza Julai watapata fursa ya kufundishwa namna bora ya kuendesha na kuzikuza biashara zao.

Pia watajiweka katika nafasi ya kuwania sehemu ya kitita cha Sh231.8 milioni kitakachowasaidia kuboresha na kuzikuza biashara ili zilete matokeo chanya kwenye jamii wakati huu ambao dunia inajikwamua kutoka katika athari za Corona. 

“Anzisha Prize imedhamiria kuwatambua na kuwasapoti wajasiriamali wadogo ambao wamekua chachu muhimu ya kuondokana na janga (la Corona),” amesema Mkuu wa Mastercard Foundation Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Daniel Hailu.

Tuzo za mwaka 2020 zilipokea zaidi ya maombi zaidi ya 1,000 kutoka kwa vijana wajasiriamali wa Afrika lakini waliopenya na kufikia hatua ya mwisho walikuwa 20 tu huku asilimia 45 wakiwa ni wanawake.

Miongoni walioshinda tuzo hizo ni David Denis (22) kutoka Tanzania, mwanzilishi wa kampuni ya Cutoff Recycle ambayo inajishughulisha na urejelezaji wa nywele za binadamu.