October 7, 2024

Nukta Africa kuwanoa wanafunzi UDSM

Ni katika mafunzo maalum ya uandishi wa habari za takwimu na uthibitishaji habari. Mafunzo hayo ya miezi miwili yanafanyika katika kituo cha mafunzo (#NuktaLab) cha kampuni hiyo kilichopo jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa Nukta Africa na wanafunzi 10 wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliani Kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kuzinduliwa kwa mafunzo maalum ya ya uandishi wa habari za takwimu na uthibitishaji habari. Picha|Nukta.


  • Ni katika mafunzo maalum ya uandishi wa habari za takwimu na uthibitishaji habari.
  • Yatatolewa katika kituo cha mafunzo cha Nukta Lab kwa miezi miwili.
  • Ni mahususi kuwaandaa wanahabari wanaochipukia kutoka vyuoni. 

Dar es Salaam. Kampuni ya Nukta Africa leo imezindua mafunzo maalum ya uandishi wa habari za takwimu na uthibitishaji habari ili kuwajengea uwezo na ujuzi wanahabari wanaochipukia kutoka vyuoni Tanzania.

Kundi la kwanza litakalonufaika na mafunzo ni wanafunzi 10 wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliani Kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanaosomea uandishi wa habari na mawasiliano ya umma. 

Mafunzo hayo ya miezi miwili yanafanyika katika kituo cha mafunzo (#NuktaLab) cha kampuni hiyo kilichopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Nuzulack Dausen akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo ni mapya nchini Tanzania na yanalenga kuwaongezea uwezo wanahabari wanaochipukia kuingia katika soko la ajira na kujiajiri. 

“Waandishi bora wanazidi kupungua, unaishije? Ni kupata ujuzi mpya. Unamaliza chuo una kitu gani unaenda kuonyesha kazini? Ni kujifunza vitu vipya,” amesema Dausen.

Dausen ambaye pia ni mkufunzi wa masuala ya data, amesema wananchi wanataka habari bora zinazowasaidia kufanya maamuzi na hiyo inawezekana kwa wanahabari kuwekeza kujifunza vitu vipya ili kuboresha uzalishaji wa maudhui. 

“Huku mtaani kuna waandishi wengi, watu wanaotusikiliza wanataka maudhui bora na huwezi kutoka sehemu yoyote ukaja kuzalisha maudhui bora, unatakiwa kujifunza vitu vipya,” amesema bosi huyo wa Nukta Afrika.

Miongoni mwa ujuzi unaoitajika ni pamoja na uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji wa habari, zana za kidijitali, nidhamu na utayari wa kujifunza vitu vipya.

Kutolewa kwa mafunzo hayo ni jitihada za Nukta Africa kutoa mchango wake katika kuwajengea uwezo Wanahabari wanaochipukia kupata ujuzi, maarifa na teknolojia ya kisasa itayohitajika katika tasnia ya habari kwa sasa.


Soma zaidi: 


Mkuu wa Mafunzo na uendelezaji wa Biashara wa Nukta Africa, Daniel Mwingira amesema mafunzo hayo ni endelevu na yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ili kuziba pengo la ujuzi linalokosekana kwenye tasnia ya habari.

Amewataka waliopata fursa ya mafunzo hayo kutumia muda wao vizuri na kujitoa ili kupata ujuzi na maarifa yanayohitajika.

Nukta Africa ni kampuni ya habari na teknolojia inayofanya kazi ya kuboresha maisha ya watu kwa kutumia takwimu na maudhui ya mtandaoni.

Inamiliki tovuti ya habari ya Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kituo cha mafunzo (#NuktaLab), inatengeneza infografia kwa ajili ya habari na biashara na kutoa ushauri wa masuala ya matumizi ya takwimu kufanya maamuzi.

Kwa taarifa zaidi, endelea kutufuatilia katika mitandao yetu ya kijamii ya Facebook, Twitter na Telegram @NuktaTanzania na @nuktatz kwa Instagram.