November 24, 2024

Soko la tumbaku laitesa wizara ya kilimo Tanzania

Baadhi ya makampuni ya tumbaku nchini hununua zao hilo kwa bei ya chini wakidai ni ya kiwango cha chini (makinikia) kisha huyapeleka nje na kuuza kwa bei nzuri.

  • Wakulima hawafaidiki na  masoko ya zao hilo.
  • Makampuni yanayonunua zao hilo huuza kwa bei ya kuu nje ya nchi.
  • Serikali yasema itahakikisha wakulima wanapata tija ya zao hilo. 

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema wizara hiyo inakibiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wakulima kukosa masoko ya uhakika ya tumbaku wakati makampuni yanayonunua zao hilo huuza kwa bei ya juu nje ya nchi.

Zao hilo hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo sigara ambazo zinatajwa kuwa na madhara ya kiafya ikiwemo kusababisha kansa ya mapafu.

Prof Mkenda amesema baadhi ya makampuni ya tumbaku nchini hununua zao hilo kwa bei ya chini wakidai ni ya kiwango cha chini (makinikia) kisha huyapeleka nje na kuuza kwa bei nzuri.

“Suala la makinikia ya tumbaku halikubaliki sasa, Serikali itahakikisha kunakuwepo ushindani wa kweli katika masoko ya tumbaku ili wakulima wetu wanufaike tofauti na ilivyo sasa,” amesema Mkenda katika kipindi cha Kumekucha cha kituo cha televisheni cha ITV leo Februari 11 jijini Dodoma. 


Zinazohusiana:


Licha ya changamoto hizo za masoko, tumbaku ni miongoni mwa mazao yanayoingiza fedha nyingi za kigeni.  

Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani (GATS) wa mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanziabar (OCGS) imeeleza kuwa, zao la tumbaku linachangia zaidi ya Sh92.5 bilioni kila mwaka katika pato la Taifa.

Sehemu kubwa ya mapato hayo ni kutokana na mauzo ya zao hilo nje ya nchi ambapo hadi kufikia mwaka 2019, Tanzania ilizalisha tani 68,147 za tumbaku kama ilivyoelezwa katika Uchambuzi wa Takwimu muhimu (Tanzania in figures 2019).

Amesema Serikali iko katika utekelezaji wa mikakati ya kuongeza tija na kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli za kilimo ikiwemo uhakika wa masoko ya mazao.

Kwa sasa kilimo kinachangia chini ya asilimia 30 kwenye pato la Taifa wakati kikiwa kimeajili zaidi ya asilimia 70 ya nguvukazi hali inayochangiwa na kuwepo tija ndogo kwenye kilimo.