October 7, 2024

Serikali yaagiza kuongezwa minara ya mawasiliano ya simu Tanzania

Agizo hilo linatokana na uwepo wa minara isiyokidhi mahitaji ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo nchini.

  • Agizo hilo linatokana na uwepo wa minara isiyokidhi mahitaji ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo nchini.
  • Hali hiyo inasababisha watu kukosa huduma ya  mawasiliano licha  ya kuwepo kwa minara iliyokamilika.
  • Serikali inaendelea na utoaji ruzuku na zabuni za kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika kata ambazo hazijafikiwa.

Dar es Salaam. Serikali imezitaka kampuni zinazotoa mawasiliano ya simu Tanzania kufanya tathmini ya utendaji wa minara ya simu na kuongeza mingine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini. 

Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew aliyekua akizungumza leo Februari 10, 2020 Bungeni jijini Dodoma amesema  kumekuwepo  minara ambayo haikidhi mahitaji ya mawasiliano ya watu na isiyofanya kazi katika maeneno mbalimbali, licha ya kukamilika kwa ujenzi wake.

Amesema pia kwenye baadhi ya maeneo kuna ongezeko kubwa la watu, jambo linalofanya minara ya simu iliyopo isikidhi mahitaji ya ongezeko hilo. 

Kutokana na changamoto hizo ambazo zinakwamisha maendeleo ya wananchi, amezitaka kampuni za simu kushughulikia tatizo hilo haraka.

“Tumeagiza watoa huduma za mawasiliano wote wafanye tathmini, wafanye utafiti wa kutosha ili waongeze uwekezaji katika maeneo hayo aidha kwa kuongeza minara au kwa kuongeza uwezo katika minara ambayo tayari ipo katika maeneo husika,” amesema Mathew. 


Soma zaidi:


Naibu waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti Maalumu, Grace Tendega aliyetaka kujua Serikali ina mikakati gani ya kutatua changamoto ya mawasiliano ya simu katika jimbo la Kalenga mkoani Iringa.

“Tatizo lilopo Mbulu vijijini ni sawa na tatizo lililopo katika Jimbo la Kalenga. Ni lini serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kawaida,” amesema Tendega katika swali lake.