October 7, 2024

Serikali yawakalia kooni wafamasia wanaokiuka maadili

Ni wale wanaokiuka maadili ya kazi zao kwa kutokuwepo katika vituo vyao vya kazi na kushindwa kusimamia majukumu yao.

  • Ni wale wanaokiuka maadili ya kazi zao. 
  • Watakiwa kujisalimisha ndani ya siku 14 ikiwa hawapo kwenye vituo vyao vya kazi. 

Dar es Salaam. Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Elizabeth Shekalaghe ametoa siku 14 kwa wafamasia wanaosimamia famasi ambazo hazipo katika maeneo yao ya kazi kujisalimisha katika baraza hilo.

Shekalaghe ametoa agizo hilo Januari 28 wakati akiongea na maafisa habari wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika ofisi zake zilizo katika jengo la Bima ya Afya Jijini Dodoma.

“Kwa wale wafamasia ambao wanasimamia famasi ambazo hazipo ndani ya  maeneo yao ya kazi, natoa siku 14 kuanzia leo, kujisalimisha Baraza la Famasi. Mtu anakaa Morogoro anasimamia famasi Dodoma, lakini taarifa alizotuletea sisi yupo Dodoma, sasa tumeshaanza kufanya ufuatiliaji maalum ili kuwabaini,” amesema Shekalaghe. 

Baraza hilo limeanza kufanya ufuatiliaji maalum ili kuwabaini wafamasia wote wanaokiuka maadili na sheria kwa kutoa taarifa za uongo za kuonekana yupo kwenye kituo fulani, wakati uhalisia anakuwa katika kituo kingine.

“Kifungu Na. 43 cha Sheria ya Famasi, Sura 311 kinaelekeza kwamba, hairuhusiwi mtu yoyote kujihusisha na biashara ya famasi kama sio mfamasia, endapo mtu huyo atahitaji kufanya hivyo, atalazimika kutafuta mfamasia ili asimamie huduma hiyo,” amesisitiza msajili huyo. 


Soma zaidi:


Amesema wamebaini kuwa kumekuwa na tabia ya wafamasia kuingia mikataba na wamiliki wa maduka ya famasi, huku wakishindwa kutekeleza majukumu yao, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utendaji wa taaluma na bado wakipokea mishahara ya usimamizi wa famasi hizo bila kufika na kutekeleza majukumu yao ya msingi.

Amesisitiza kuwa kanuni ya 13 ya Kanuni za Usajili wa Famasi imeelezea kuwa, kutofika kwa mfamasia katika famasi ni moja ya sababu za kufutwa kwa kibali cha uendeshaji wa huduma hizo kwa sababu ya kukosa usimamizi.  

Aidha, Shekalaghe amesisitiza kuwa, dawa si biashara, bali ni huduma ambayo inapaswa kusimamiwa kwa weledi wa hali ya juu na mtaalamu aliyepewa jukumu hilo kisheria na  mwenye vigezo na maadili ya utoaji huduma hiyo.

“Sitakubali kuona uzembe na kutowajibika kwa wafamasia wachache huku wakiendelea kuwaweka wananchi katika hatari ya kupata athari dhidi ya matumizi holela ya dawa. Hilo halikubaliki,” amesisitiza.