November 24, 2024

Kiswahili kuanza kufundishwa vyuo vya Ethiopia

Kitaanza kufundishwa katika Chuo Kikuu Cha Addis Ababa nchini humo.

  • Ni baada ya Mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania na Rais wa Ethiopia.
  • Kitaanza kufundishwa katika Chuo Kikuu Cha Addis Ababa nchini humo.
  • Walimu wa Kiswahili kuneemeka na fursa hiyo.  

Dar es Salaam. Huenda itakua ni kicheko kwa wabobezi wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania, baada ya Serikali kuingia makubaliano na Ethiopia ya kuanza kufundishwa kwa lugha hiyo katika Chuo Kikuu Cha Addis Ababa nchini humo.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Januari 25,2020 kati ya Rais John Magufuli na Rais wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Watu wa Ethiopia, Sahle – Work Zewde aliyekuwepo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku wilayani Chato Mkoani Geita.

“Leo tumezungumza naye amesema hili swala wala halina tatizo atapenda kupata walimu watakaoshiriki kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu Cha Addis Ababa na mimi nimemshukuru sana Mheshimiwa Rais,” amesema Rais Magufuli, baada ya kumaliza mazungumzo na mgeni wake.

Kiswahili ni lugha ya Taifa ya Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, ambapo kimekuwa kiungo muhimu cha shughuli mbalimbali ikiwemo biashara na utamaduni duniani.  


Soma zaidi:


Rais Zewde amesema juhudi hizo ni muendelezo wa juhudi zilizokuwepo za kuifanya lugha ya Kiswahili kama lugha ya bara la Afrika.

“Tulikuwa na mchakato wa kutaka Kiswahili kiwe lugha inayotumika Afrika. Nashukuru sana na tutakuwa tayari kuwapokea walimu kutoka Tanzania kwa ajili ya kufundisha Kiswahili Ethiopia,” ameeleza Rais wa Ethiopia.

Pamoja na fursa hiyo kwa walimu wa Kiswahili wa Tanzania, marais hao pia walipata muda wa kujadili makubaliano katika sekta za mifugo, uwekezaji, utalii na ulinzi ambayo lengo lake ni kuendelea kunufaisha nchi hizo mbili zilizo na mahusiano mazuri kwa muda mrefu.

Pia Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kinazidi kuchanja mbuga hadi jumuiya za kimataifa.