October 7, 2024

Yakuzingatia kabla hujasaini mkataba wa ajira

Ni pamoja na kufahamu jina la muajiri, muda wa mkataba na majukumu ya kazi yako.

  • Ni pamoja na kufahamu jina la muajiri, muda wa mkataba na majukumu ya kazi yako.
  • Kuelewa mkataba kutakuepusha na matatizo yasiyo ya lazima ikiwemo kufanya kazi muda mwingi. 

Mkataba wa ajira ni aina ya mkataba ambao unatoa uhusiano kati ya muajiri na muajiriwa, pia majukumu baina ya pande hizo mbili. Kabla ya kuajiriwa sehemu yeyote ile lazima muajiriwa apewe mkataba ambao atasaini. 

Kupitia mkataba huo muajiriwa ataweza kutambua vyema majukumu yake ya kikazi pamoja na wajibu wake mbele ya muajiri wake. Mkataba unatoa majukumu ya kisheria mabayo yanapaswa kutekelezwa vyema baina pande zote mbili za mkataba huo. Mikataba yote ya ajira inapaswa kukidhi vigezo vilivyowekwa kisheria za mikataba na sheria za kazi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo basi ni vyema kwa muajiriwa kuelewa na kufahamu vyema vipengele vyote vya mkataba wake kabla ya kusaini mkataba huo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima. 

Vifuatavyo ni vipengele muhimu vya mkataba wa ajira ambavyo muajiriwa anapaswa  kuzingatia kabla ya kusaini mkataba wake:

  1. Jina la muajiri wako

Huyu ndiyo mhusika mkuu wa mkataba wa kazi, hivyo muajiriwa anapaswa kutambua kuwa anaajiriwa na nani . Kwa siku za karibuni kumekua na mawakala wa ajira ambao wanaajiri watu kwa niaba ya makampuni mengine, hivyo ni vema kujua kama unaajiriwa na kampuni husika au wakala wa ajira. Hii itakusaidia kujua nani ni muajiri wako na kuweza kujua mtekelezaji wa majukumu yako. Kushindwa kumtambua muajiri wako itasababisha kutokumtambua mtu sahihi wa kumuwajibisha pale ambapo masharti ya mkataba yatashindwa kutekelezeka.


Soma zaidi: 


  1. Aina ya mkataba wako na muda wa mkataba

Hapa utaweza kutambua kama umeajiriwa kwa mkataba wa kudumu au muda ama wa kazi maalumu. Kipengele hiki lazima kiseme aina ya ajira yako mbele ya muajiri. Ikiwa mkataba utakua umeandikwa lakini hauonyeshi ukomo wa muda wa ajira yako basi inatosha kusema  kuwa utakua umeajiriwa kwa muda wa kudumu mpaka kifo chako. Kutambua kundi ulilopo ni muhimu kuweza kuepusha utata mbele ya vyombo vya sheria. Muajiriwa anatakiwa kutambua kwa umakini kipengele hiki kabla ya kusaini.

  1. Malipo yako

Kipengele hiki lazima kionyeshe kuwa unalipwa kiasi gani kama ujira wa kazi yako. Lazima kionyeshe kama unalipwa kwa mwezi au wiki au kwa saa. Hapa lazima ioneshe kuwa mshahara ghafi ni shilingi ngapi na mshahara baada ya makato ni shilingi ngapi. Pia lazima ibainishe ikitokea kuna saa za ziada utalipwa kiasi gani cha pesa kwa kila saa. Ni vyema ujue kutofautisha mshahara ghafi na mshahara baada ya makato ili uweze kutambua vizuri haki yako ya malipo  


  1. Muda wa kazi

Mkataba lazima ubainishe kuwa utafanya kazi kwa saa ngapi, hii itakuwezesha kujua kuwa utaingia kazini saa ngapi na kutoka saa ngapi. Uwepo wa muda unakufanya kutambua vizuri kuwa saa itakayozidi kama utalipwa “overtime”. Kushindwa kutambua muda wa kazi itakufanya ufanye kazi kwa muda mrefu kinyume cha sheria, hakikisha unatambua muda wako wa kazi kuepusha kilio cha saa nyingi za kazi.

Mkataba wa ajira ni aina ya mkataba ambao unatoa uhusiano kati ya muajiri na muajiriwa, pia majukumu baina ya pande hizo mbili. Picha| Shironovos.

      5.Kuvunjika kwa mkataba au ukomo wa mkataba

Kipengele hiki kinabainisha ni tukio gani au kitu gani ambacho kitahitimisha safari ya mahusiano ya kimkataba kati ya muajiri na muajiriwa. Kipengele hiki huwa kinasema bayana kukoma kwa mkataba na matokeo ya kukoma kwa mkataba wa ajira. 


  1. Majukumu yako ya kazi

Lengo kuu la wewe kuajiriwa ni kutimiza majukumu kadhaa ya muajiri wako, mkataba wako lazima ubainishe kuwa majukumu yako ya kikazi ambayo ndiyo yatakua msingi wako wa kazi za kila siku. Kushindwa kutekeleza majukumu yako ya kila siku kunaweza kusababisha kuvunjika kwa mkataba wako.

Ni vyema kujua kipi unatakiwa kufanya na kipi hautakiwi kufanya kama muajiriwa wa sehemu husika. Kutambua majukumu yako itakuondolea lawama zisizo za msingi eneo la kazi. 

Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,

 Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini

Twiter@Hamzaalbhanj

Instagram@Hamzaalbhanj

Simu: 0717521700