November 24, 2024

Wagonjwa wapya wa saratani kuongezeka kwa asilimia 50 Tanzania

Kwa sasa, Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani wapatao 50,000.

  • Kwa sasa, Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani wapatao 50,000. 
  • Idadi hiyo itaongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030
  • Serikali yawataka wananchi kupima afya mara kwa mara kujua hali zao. 

Dar es Salaam. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani nchini Tanzania, jambo linalohitaji hatua za haraka kutatua changamoto ya ugonjwa huo. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima amesema kwa sasa, Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani wapatao 50,000. 

Dk Gwajima amesema kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia  tafiti za saratani (IARC), takwimu za hapa nchini  za 2018 zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ni 14,028 sawa na asilimia 33.3 ya wagonjwa wote nchini.

“Saratani kama moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza inashika nafasi ya tano kwa wanaume na ya pili kwa wanawake kwa kusababisha vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini,” amesema waziri huyo Januari 19 wakati wa uzinduzi wa idara ya magonjwa ya saratani, huduma za patholojia na mkataba wa mteja kwenye hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma. 

Saratani zinazoongoza kwa wanawake ni mlango wa kizazi na saratani ya matiti huku kwa wanaume ni saratani za tezi dume, koo, kichwa na shingo.

Aidha, Dk Gwajima amesema magonjwa ya saratani yanatibika iwapo tu mgonjwa atawahi kupata tiba katika vituo vya afya vinavyotoa huduma hiyo. 

“Nitoe rai kwa wananchi, tujenge tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara ili ikibainika kuwa tuna changamoto za kiafya basi tuanze matibabu bila kuchelewa,” amesisitiza Dk Gwajima. 


Soma zaidi: 


Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zaidi ya asilimia 75 ya wagonjwa wa Saratani hufika katika Vituo vya matibabu wakiwa wamechelewa sana na kuwawia vigumu madaktari kutibu na kuponya ugonjwa huo.

Serikali kwa kushirikiana na wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali imeendelea kuhakikisha inapambana na magonjwa ya saratani, ambapo katika kukabiliana na hilo Serikali imefunga mashine mbili za kisasa za tiba ya saratani kwa njia ya mionzi aina ya LINAC katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambazo zimeanza kutoa huduma tangu Septemba, 2018. 

Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Serikali imeanzisha vituo takribani 624 ambavyo huweza kugundua na kutibu mapema saratani ya mlango wa kizazi.