November 24, 2024

Usiyoyafahamu kuhusu wasichana watatu bora matokeo kidato cha nne 2020

Mabinti hao sio “vipanga” tu wamebarikiwa na vipaji vinavyoambatana na ubora wao darasani.

  • Wasichana wote wametokea shule ya Sekondari ya Canossa.
  • Ndoto zao zitaongeza wanawake katika shughuli za kisayansi na teknolojia.
  • Mabinti hao sio “vipanga” tu wamebarikiwa na vipaji vinavyambatana na ubora wao darasani.

Dar es Salaam. Kuwa mwanafunzi bora kitaifa katika matokeo ya mtihani ni jambo ambalo kila mwanafunzi analitazamia. Lakini ni wachache wanaopata fursa hiyo ya kuingia katika orodha ya 10 bora. 

Katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2020 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) hivi karibuni, pia imetolewa orodha ya 10 bora ya wasichana waliofanya vizuri kitaifa. 

Orodha hiyo ya wasichana 10 bora imetawaliwa na watahiniwa kutoka shule ya Canossa iliyopo jijini Dar es Salaam ambayo imefanikiwa kuingiza wasichana wanne walioshikilia nafasi nne za kwanza.

10 bora hiyo imeongozwa na Justina Gerald akifuatiwa na wenzake watatu Layla Atokwete, Lunargrace Celestine na Catherine Mphumuhila aliyeshika nafasi ya nne. Nafasi ya tano imeenda kwa Happyness Matata kutoka shule ya Musabe Girls ya jijini Mwanza huku Debora Mwenda wa St Francis Girls ya jijini Mbeya akishika nafasi ya sita.

Mwanafunzi bora wa kike katika nafasi ya saba ni Rose Kaale wa Precious Blood (Arusha) anayefuatiwa na Wendo Manyelezi kutoka Marian Girls ya mkoani Pwani katika nafasi ya nane. 

Nafsi ya tisa imeshikiliwa na Bellin Mungunasi wa St Francis huku orodha hiyo ikifungwa na Nancy Mung’azo wa St Francis

Huenda umepata nafasi ya kusoma makala mbalimbali kuwahusu wasichana hao lakini yapo baadhi ambayo bado hauyafahamu hasa katika malengo yao ya mbeleni, jitihada wanazofanya kuyafikia na maisha yao nje ya darasani.

Na hii ndiyo ana kwa ana kati ya Nukta Habari (www.nukta.co.tz) na wanafunzi hao:

Bila shaka umesoma mengi kuhusu mabinti hao lakini yapo usiyoyafahamu. Picha| Rodgers George & Layla Atokwete.

Kwanini Canossa na siyo kwingine

Bila shaka jambo hilo limewashangaza wengi kwa shule ya Canossa kuingiza wasichana wanne katika orodha hiyo. Lakini siyo bahati mbaya kwa sababu shule ilifanya kazi kubwa ya kufundisha watahiniwa. 

Kwa mujibu wa Mkuu wa shule hiyo, Mtawa Irene Nakamanya, kilichowasaidia watoto wa shule hiyo ni hofu ya Mungu ambayo imejengwa ndani yao.

Licha ya watoto hao kutokuhudhuria masomo kwa zaidi ya miezi miwili katika kipindi cha Corona, bado wameweza kufanya vizuri katika matokeo yao nje ya matarajio yao.

“Tunamshukuru Mungu. Amekuwa mwaminifu. Justina alikuwa akiongoza wenzake darasani na Layla alikuwa mwanafunzi bora katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili,” amesema Nakamanya.

Hata hivyo, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanya mahojiano na wasichana hao wanne waliong’ara katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2020. 


Historia ilivyowabeba

Msemo wa siku njema huonekana asubuhi haukuenda mbali na matokeo ya binti hawa ambao kuanika mabanda kwenye karatasi zao za matokeo siyo jambo geni.

Justina ambaye ameongoza orodha hiyo amekuwa akipata alama “A” tangu alipokuwa darasa la saba wakati akisoma Shule ya Msingi Tusiime jijini Dar es Salaam. 

Layla Atokwete aliyeshika nafasi ya pili kwa wasichana wote alikuwa mwanafunzi bora kitaifa katika matokeo ya kidato cha pili mwaka 2018 akiwa na “mabanda” katika masomo yake yote.

Naye Lunargrace, hayupo mbali na watatu hao kwani naye mtihani wa kidato cha pili alikuwa na alama A katika masomo yote 12 aliyofanyia mtihani.

“Nilipata alama D katika somo la “additional mathematics” katika mtihani wangu wa Mock. sikukata tamaa, nilimfuata mwalimu wangu na alinifundisha na wanafunzi wenzangu hawakutaka kuniacha nibaki nyuma. Nimepata alama A katika masomo yote,” amesema Justina akiongea na Nukta Habari.

Tutegemee kuwaona wapi miaka 10 ijayo?

Kufikia malengo yao kielimu kwa ngazi ya Shahada ya Uzamiri inakadiriwa kutumia hadi miaka nane ikiwa ni muda watakautumia wakiwa kidato cha tano na sita pamoja na chuo kikuu

Kwa Justina Gerald ambaye ni mwanfunzi bora wa kike katika matokeo hayo yaliyotangazwa wiki iliyopita, ndoto yake ni kuwa mhandisi wa mafuta na gesi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa vizuri katika matumizi ya nishati safi.

“Kufikia hapo nitaendelea kuweka juhudi katika masomo. Nitakazana katika masomo ya sayansi ili nifikie malengo yangu,” Justina ameiambia Nukta.

Kwa upande wa Layla Atokwete, yeye amesema ndani ya miaka hiyo atakuwa daktari bingwa wa masuala ya ubongo au mifupa.

“Ni kazi ambayo ina uhitaji mkubwa hapa nchini na duniani kote na hivyo nimeamua kuwasaidia watu kwa namna hiyo,” amesema binti huyo.

Lunargrace Celestine ambaye ameshika nafasi ya tatu kwa wasichana na nafasi ya 10 kitaifa, yeye ana ndoto ya kuwa mtaalamu wa masuala ya teknolojia za filamu.

Furaha ya binti huyo ni kufanya kazi za filamu zilizo na ubora wa kimataifa kwa kutumia teknolojia ya juu.

“Kwa sasa ninafanya uchunguzi na ninasoma sana kufahamu masomo yanayotakiwa kusomwa ili nifikie malengo hayo,” Lunargrace ameiambia Nukta.


Hata mtaani wako vizuri

Kila mtu anapenda kufanya jambo fulani mbali na masomo na kwa mabinti hawa, huwa na mambo ambayo hupendelea kuyafanya pale wanapokuwa nyumbani.

Justina amesema yeye anapenda kusoma vitabu, kucheza muziki na awali alikuwa akijifunza kupiga kinanda lakini alikatisha mafunzo hayo kwa sababu ya shule.

“Endapo nikija kupata muda nitaanza kujifunza tena kupiga kinanda. Sina sauti ya uimbaji lakini bado nitajifunza kupiga kinanda,” amesema Justina huku akitabasamu.

Kwa Lunargrace, yeye hutumia muda wake mwingi kuchezea kompyuta na anapochoka, hutumia muda wake kushika penseli na kuchora michoro mbalimbali ikiwemo ya watu na katuni.

“Nimekuwa nikichora tangu nilipokuwa mdogo. Huwa ninafanya hivi nikiwa nyumbani na nikiwa nimemaliza kazi,” ameeleza Lunargrace huku akionyesha baadhi ya picha alizozichora.

Wakati Lunargrace akipendelea kuchora, mwenzake Layla kucheza michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa rede ndiyo shughuli yake muhimu. 

“Pia ninacheza mpira wa kikapu,” amesema Layla.


Unafanya nini mara baada ya kuamka?

Watu wengi hufikiri kuwa mabinti ambao “wanatusua” darasani hawapo vyema katika kazi zingine za nyumbani.

Hai ni tofauti kwa Justina ambaye akipika pilau na rosti ya kuku, nyumba nzima hunyoosha mikono na Lunargrace ambaye akiamka hufurahia kumsaidia mama yake kazi za nyumbani.

“Nikiamka huwa nafanya usafi na kisha ninasaidia kuwalisha binamu zangu chakula na huwa ninamwambia dada aniachie jiko nipike mara moja moja,” ameeleza Justina.


Soma zaidi:


Wazazi nao wala kiapo cha kutimiza ndoto za watoto wao

Mama mzazi wa Justina Gerald, Edna Majaliwa amesema yupo tayari kutoa mchango wake wa hali na mali katika kuhakikisha mtoto wake anafikia ndoto zake. 

Katika mazungumzo yake na Nukta kwa njia ya simu ya video, mama huyo amesema ataendelea kumshauri na kumsaidia binti yake hadi pale atakapoona mafanikio yake.

Naye baba wa Lunargrace, Greyson Celestine amesema anatambua utundu wa mtoto wake katika masuala ya kompyuta. 

Kwa nafasi yake amesema atahakikisha mtoto wake anapata elimu bora kuanzia ngazi aliyopo itakayomuwezesha kufikia ndoto yake ya kuwa mteknolojia wa masuala ya filamu.

Khalfan Atokwete, ambaye ni baba wa Layla amesema binti yake anafahamu nini anataka maishani mwake na hivyo hatokuwa na kazi ngumu sana ya kumwekekezea ni wapi anende. 

Licha ya hilo, amesema ataendelea kuwepo kama msaada pale binti yake anapokwama na ataendelea kumpatia ushauri unaostahili.

“Hata kwa watoto ambao hawajafanikiwa kupata alama nzuri, wazazi wasiwatenge watoto wao na kuwanyooshea vidole kuwa wamefeli.

“Wasitumie neno kufeli kwani kuna mengi katika maisha mbali na mitihani. Kuna kipaji cha mwanao, kivumbue na ukikuze kitamsaidia mbeleni,” amesema Edna Majaliwa, mama mzazi wa Justina.