St Francis yaendeleza ubabe matokeo kidato cha nne 2020
Imeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo hayo huku watahiniwa wake 79 kati ya 90 wakipata daraja la kwanza la pointi saba.
- Yapanda hadi nafasi ya kwanza kitaifa kutoka nafasi ya pili mwaka 2019.
- Watahiniwa wake 79 kati ya 90 wamepata daraja la kwanza la pointi saba.
- Haijawahi kutoka 10 bora tangu mwaka 2012.
Dar es Salaam. Ni miaka tisa sasa wamebaki katika ubora ule ule bila kushuka. Ni wanafunzi wa shule ya St. Francis Girls ya jijini Mbeya waliodhihirisha ubora wao katika matokeo ya kidato cha nne tena mwaka 2020.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) yaliyotangazwa jana (Januari 15, 2021), shule hiyo imeendeleza ubabe wake kwa kwa kushika nafasi ya kwanza kutoka ya pili iliyoshika katika matokeo ya mwaka 2019.
Shule hiyo wakati wote imeendelea kuogelea katika 10 bora kitaifa huku ikionyesha dalili za kutokutoka kabisa.
Mathalan, kuanzia mwaka 2012 haijawahi kutoka kwenye orodha hiyo na imekua ikipambana kushika nafasi ya kwanza kitaifa kama ilivyofanya katika matokeo ya mwaka 2020.
Kwa miaka minne yaani mwaka 2012, 2013, 2017 na mwaka 2018 ilishika nafasi ya kwanza kitaifa. Mwaka 2016 ilikuwa ya pili kitaifa , mwaka 2015 ilikuwa ya tatu kitaifa na 2014 ilishika nafasi ya nne kitaifa.
Shule hiyo ya inayomilikiwa na Kanisa Katoliki imeweza kubaki katika ubora ule ule ambao shule za sekondari zaidi ya 3,000 zimeshindwa kufikia baada ya kung’ang’ania katika shule 10 bora huku ikivunja rekodi yake yenyewe ya kuwa na wanafunzi wengi wanaopata daraja la kwanza la alama saba.
Bado watahiniwa wake wanatikisa ufaulu wa madaraja
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (mwaka 2018 hadi 2020) wanafunzi 271 walihitimu kidato cha nne katika shule hiyo na wote walifaulu kwa daraja la kwanza huku kukiwa hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la II, III, IV wala 0.
Upekee mwingine ni kuwa kati ya wahitimu 271 wa kipindi hicho,177 walipata daraja la kwanza la alama saba ikiwa ni daraja la juu kabisa la ufaulu huku walibakia wakipata daraja la kwanza la kuanzia alama nane hadi 17.
Ukilinganisha na Shule ya Sekondari ya Iliboru iliyoshika nafasi ya pili katika matokeo ya mwaka 2020, haijaweza kuifikia St Francis badala yake katika kipindi hicho miaka mitatu ilikuwa na wanafunzi 74 waliopata daraja la kwanza la pointi saba.
Matokeo ya mwaka 2020
Pia uchambuzi wa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2020 uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) unabainisha kuwa wanafunzi 79 kati ya 90 waliofanya mtihani huo mwaka jana wamepata daraja la kwanza la pointi saba ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 22 zaidi ya wale waliopata kiwango hicho mwaka 2019.
Mwaka 2019 wanafunzi 57 kati ya 91 walifanikiwa kupata daraja la kwanza la pointi saba ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 16 ukilinganisha na mwaka 2018.
Zinazohusiana:
Siri ya mafanikio ni nini?
Akiongea na Nukta Habari, Mkuu wa Shule ya St Francis, Mtawa Veena Vas amesema ufaulu wa mwaka huu unatokana na kazi kubwa waliyofanya ya kuwawekeza mazingira mazuri watahiniwa.
Amesema uwekezaji huo umesaidia kupanda hadi nafasi ya kwanza kitaifa.
“Tumefanya kazi kubwa sasa ni muda wa Mungu kutupatia tuzo ya kazi tuliyoifanya,” amesema Mtawa Vas huku akijawa na furaha kwa shule yake kupata ushindi huo.
Licha ya kufanya vizuri, mkuu huyo wa shule amesema watahiniwa wake hawajafanya vizuri katika somo la fizikia, hivyo watafanya tathmini ili kuongeza ufaulu mwaka ujao.
Katika matokeo yaliyotolewa na Necta yanaonyesha watahiniwa wa shule zote waliofanya mtihani huo mwaka jana hawajafanya vizuri katika masomo ya Fizikia na Hisabati ambapo ufaulu uko chini ya wastani wa kitaifa.