Usikose kutembelea sehemu hizi ukiwa Zanzibar
Kuanzia hoteli za kipekee, fukwe za kufurahisha na vijiji vya kustaajabisha ni kati ya chaguzi unazotakiwa kufanya unapokuwa Zanzibar.
- Kuamua uende kutembea wapi unapofika Zanzibar inaweza kuwa mtihani mgumu kwa wengi
- Uwepo wa sehemu lukuki za kutembelea inaweza kukausha uhai wa pochi yako lakini kwa utalii ambao hautojutia.
- Kuanzia hoteli za kipekee, fukwe za kufurahisha na vijiji vya kustaajabisha ni kati ya chaguzi unazotakiwa kufanya unapokuwa Zanzibar.
Dar es Salaam. Mara moja moja siyo mbaya kubadilisha mazingira kwa kutembelea sehemu mpya kwa ajili ya kutuliza akili na kuuacha mwili wako ufurahie maisha nje ya kazi.
Kwa Tanzania, unaweza kufanya hivyo kwa kutembelea mbuga za wanyama, fukwe na hata kupanda milima mbalimbali akiwemo mlima mrefu zaidi Afrika, Kilimanjaro.
Pamoja na hayo yote, unaweza kuangazia kutembelea visiwa na kujionea maajabu yaliyozungukwa na bahari ya Hindi kuanzia samaki wa kufurahisha macho huku upepo wa bahari ukiendelea kuufurahisha mwili wako na jua la kutania likiiangaza ngozi yako.
Endapo una mpango wa kwenda Zanzibar, hizi ni baadhi ya sehemu unazoshauriwa kuzitembelea:
Mgahawa wa The Rock
Yapo mengi ya kustaajabisha kila jina la mgahawa huo linapotajwa lakini zaidi ni kuwa mgahawa huo umezungukwa na maji ukiwa karibu na ufukwe na itakuhitaji kupanda mtumbwi kuufikia.
Bei za kuvinjari mgahawa huo uliopo katika kijiji cha Michamvi Pingwe siyo kubwa sana lakini kwa kifupi ni unahitaji walau Sh70,000 kupata mlo na kinywaji cha mtu mmoja.
Kama wewe ni mdau wa vyakula vya baharini vikiwemo pweza, kaa na vinginevo, huenda ukawa mteja wa mgahawa huo unaotengeneza vyakula vya asili ya Kiitaliano.
Pia, mgahawa huo ni sehemu nzuri kwa wanandoa kufanyia sherehe zao. Unataka kumpatia mpenzi wako harusi ya ndoto yake? Usiseme haufahamu.
Kwa kifupi ni unahitaji walau Sh70,000 kupata mlo na kinywaji cha mtu mmoja. Picha| hefs in Africa.
Safari za Nungwi, Paje na Jambiani
Kuna raha gani ya kutembelea mahala usipate nafasi ya kukutana na wazawa wa sehemu hiyo na kujifunza mambo mapya?
Kuanzia kuifahamu historia ya wazawa wa Zanzibar, kujifunza tamaduni za lugha, chakula na mavazi ya Wanazanzibar, utahitaji kufika katika vijiji hivyo vinavyopatikana Unguja.
Kwa wageni wanaopenda michezo, watafurahia mchezo wa “kitesurfing” ambao huusisha kucheza baharini kwa kishada na ubao maalumu (surf board).
Mchezo huu huwa bomba zaidi katika fukwe za Zanzibar kutokana na usafi wa maji na upepo mwanana.
Kuogelea katika mapango ya Kuza
Kuogelea baharini siyo kitu kigeni kwa watu wengi lakini kuogelea kwenye mapango ya Kuza amabyo yana maji yenye kina cha hadi futi nane bila shaka humpatia mtu msisimko pale anaposikia hilo linawezekana ukiwa Zanzibar.
Mapango hayo ambayo yapo Jambiani, yanahitaji utoboe mfuko kidogo kwani kwa mujibu wa wadau wa kitalii wa tripadvisor, utahitaji Sh269,900 kupata saa tano ya kufurahia muda wako katika pango hilo.
Pesa hiyo inajumuisha chakula cha mchana, maji na usafiri.
Hata hivyo, gharama hiyo inaweza kupungua ama kupanda kulingana na wingi wa watu na vikundi vinavyokwenda huko.
Soma zaidi:
- Kiswahili kinavyotumika kukuza utalii Marekani
- Unavyoweza kuepuka changamoto za usafiri wa ndege
- Kabila la Bodi: Wanaume wanavyoshindana kupata unene
Hoteli ya Manta, Pemba
Yapo mengi yanayoweza kukustaajabisha katika hoteli hii lakini kubwa zaidi ni uwepo wa chumba kimoja ambacho ni tofauti na vyumba vingine.
Chumba hicho kipo chini ya bahari na madirisha yake yana uwezo wa kukuruhusu utazame viumbe bahari kwa ukaribu bila haja ya kuogelea.
Fikiria ni mangapi unaweza kufanya ukiwa katika hoteli hii ambayo madirisha ya chumba hicho kilichopo chini ya maji ni ya kioo. Mbali na kuona wanyama bahari wa kila aina, itakupatia nafasi ya kupumzika na kusahau tabu za dunia kwa muda.
Sehemu zingine ambazo unaweza kufurahia unapotembelea Zanzibar ni Forodhani ambapo utajipatia vyakula vya Pwani katika mji Mkongwe almaarufu kama Stone Town.
Sehemu zingine ni pamoja na Ngome Kongwe, misitu ya Jozani na Ngezi ambapo utajionea nyani aina ya Red Colobus na tumbili pamoja na kutembelea mashamba ya viungo.