Jinsi ya wazazi wanavyoweza kuwasaidia wanafunzi kidato cha kwanza
Ni pamoja na kuendelea kufuatilia mwenendo wa mtoto wako akiwa shuleni kitaaluma na kinidhamu.
- Ni pamoja na kuanza kuwekeza kwa ajili ya elimu ya mtoto wako kwa kuweka akiba.
- Pia, kuendelea kufuatilia mwenendo wa mtoto wako akiwa shuleni kitaaluma na kinidhamu.
- Msaidie kusoma kile anachokipenda.
Dar es Salaam. Ni mwezi Januari, mwanzo mwa mwaka 2021. Wanafunzi wanarejea shuleni baada ya likizo ya mwisho wa mwaka 2020.
Kwa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi yaani darasa la saba, sasa wameingia katika hatua nyingine ya elimu ya sekondari. Bado wana safari ndefu kufika elimu ya juu.
Wanawajibika kusoma kwa bidii kufikia ndoto zao. Lakini wazazi nao wana jukumu kubwa kuhakikisha watoto wao walioingia sekondari wanatimiza ndoto zao.
Mbali na kulipa ada, mzazi ana jukumu gani lingine kwa mtoto wake akiwa shuleni?
Kuimarisha mawasiliano na walimu
Baadhi ya wanafunzi wamechaguliwa kujiunga na shule za mbali na nyumbani kwao au bweni. Jambo hilo linatakiwa kutokupuuzwa na mzazi yeyote kwani katika umri ambao mtoto anakua, kunaweza kuwepo na mabadiliko mbalimbali.
Daniel Meshack ambaye ni mkazi wa Mwanza ameiambia Nukta kuwa, katika kipindi hicho, mtoto hukutana na rafiki wapya ambao wanaweza kumjengea au kumharibia mwelekeo wake wa kimasomo.
“Mimi mtoto wangu hajachaguliwa mbali sana na nyumbani lakini umbali anaotembea kwenda shule kuna mengi. Kuna wanaume, wasichana wadogo walioacha shule na majaribu mengi.
“Mzazi ukiacha kumfuatilia mtoto wako utashangaa unaletewa mjukuu nyumbani,” ameeleza Meshack ambaye binti yake ameingia kidato cha kwanza.
Meshack anashauri wazazi kuwa na mawasiliano na walimu hasa wa darasa kujua mahudhuria ya watoto wao shuleni, nidhamu na hata kuwajengea mahusiano mazurri watoto wao na walimu.
“Kuna walimu wengine wanaweza kuwa wakarimu kwa mtoto wako kwa sababu unawasiliana nao vizuri. Wanakuwa wanakusaidia hata kumshauri mtoto wako hata kama haupo karibu, siku zinaenda,” ameeleza baba huyo wa watoto watatu.
Elimu ya mtoto wako ni muhimu kumjenga kifikra, hivyo una wajibu wa kufuatilia kwa karibu maendeleo yake. Picha|Tehama
Kufuatilia ubora wa shule aliyokwenda mtoto
Serikali imefanya kazi yake ya kuhakikisha mtoto wako anaingia kidato cha kwanza. Nafasi iliyobaki ni yako ya kuhakikisha kuwa malengo ya mtoto wako yanatimia ikiwa ni pamoja na kujua uwezo wa shule ambayo mtoto amepangiwa.
Mathalan, malengo ya mtoto wako yanaweza kuwa ni kuwa daktari na hivyo kuhitaji msingi mzuri wa masomo ya sayansi. Endapo atashindwa kuupata msingi huo kuanzia kidato cha kwanza, atapata shida mbeleni.
Kati ya wazazi walioshindwa katika hilo ni Lydia Limo ambaye mtoto wake alitamani kuwa mhandisi wa kompyuta lakini alienda shule ambayo somo la kompyuta halipo na hivyo kuishia kufanya kazi ambayo hakuwahi kuifikiria.
Limo ameiambia Nukta kuwa, mzazi anatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha ndoto za mtoto wake zinatimia hasa kama ana uwezo.
“Mimi tangu anamaliza darasa la saba aliniambia angependa kusoma mambo ya kompyuta lakini alienda shule gani sijui na kompyuta haina, sayansi hayafundishwi vizuri matokeo ameamua kusoma somo ya ualimu,” ameeleza Limo.
Soma zaidi:
- Jinsi ya kukabiliana na changamoto unapoanza mwaka 2021
- Faida za kuishi karibu na sehemu ya kazi
- Sababu za akaunti ya Trump kufungwa rasmi
Maandalizi ya kiuchumi ni muhimu
Hakuna mzazi anayeifahamu kesho yake. Leo unaweza kuwa na kazi nzuri inayotosha kulipia ada ya mtoto wako kwa mwaka mzima. Itakuaje kama mwezi ujao ukaamka ajira hiyo isiwepo tena? Je ndiyo utakuwa mwisho wa elimu ya mtoto wako?
Flora Harrison, mwalimu kutoka shule ya Maitarya jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kila shule imetoa mgawanyo wa malipo ya ada ya mtoto.
Ili kuepukana na mtoto wako kusimamishwa masomo kwa sababu ya ada, ni vyema ukaweka akiba au ukalipa ada ya mwaka mzima.
“Siyo lazima uikusanye yote, lakini unaweza kuwa unaweka kidogo kidogo walau ufikishe nusu ya ada ya mtoto wako ili hata mhula mwingine unapoanza na ada ikitakiwa, una pakuanzia,” amesema mwalimu huyo.
Kuwasimamia watoto wa shule za kutwa kujisomea
Kwa watoto wa shule za bweni, wengi wao huwa na vipindi vya kujisomea baada ya chakula cha usiku lakini huenda hali ni tofauti kwa watoto wa shule za kutwa.
Kwa baadhi ya shule huwa na kitabu cha mawasiliano kati ya mzazi na mwalimu kinachoainisha kazi, ratiba za vikao na vinginevyo. Wazazi wanatakiwa kuwashinikiza watoto wao kupata muda wa kujisomea baada ya shule ili kuelewa walichofundishwa.
“Siyo anachati tu! Apate muda wa kujisomea na kujikumbusha alichofundishwa shuleni,” amesema Harrison.
Usiache kutuma habari hii kwa mzazi ama mtu anayeweza kuisoma na ikamsaidia. Kutokana na wingi wa majukumu, huenda baadhi yao husahau vitu wanavyotakiwa kuvizingatia.