Magufuli aiomba China kuisamehe Tanzania madeni
Miongoni mwa madeni ni lile la ujenzi wa reli ya Tazara miaka 50 iliyopita
- Miongoni mwa madeni ni lile la ujenzi wa reli ya Tazara miaka 50 iliyopita
- Pia aiomba China kuisaidia Tanzania katika miradi ya umeme wa maji mkoani Njombe na barabara visiwani Zanzibar.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiomba Serikali ya China kuisamehe Tanzania baadhi ya madeni likiwemo la ujenzi wa reli ya Tazara iliyounganisha nchi ya jirani ya Zambia iliyojengwa miaka 50 iliyopita.
Dk Magufuli, aliyekua akizungumza leo Januari 8, 2020 baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi katika Wilaya ya Chato mkoani Geita amesema nchi hizo mbili ni marafiki na China ni taifa tajiri duniani.
Akitaja madeni hayo, Rais amesema deni mojawapo ni la Dola za Marekani milioni 15.7 (Sh36.5 bilioni) ambalo Tanzania ilibeba wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara ambayo imekuwa kiungo muhimu kwa mizigo na biashara inayofanyika katika nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Lakini kuna deni la nyumba la maaskari wetu ambao wamekuwa wapiganaji wazuri na ambao wameshiriki katika mission (shughuli) mbalimbali za kimataifa ambapo ni karibu dola milioni 137 (Sh317.7 bilioni) na tumeshalipa zaidi ya dola milioni 164 (Sh380.4 bilioni),” amesema Magufuli akibainisha kuwa mazungumzo yake na Yi yalikuwa ni mazuri.
Deni lingine ni la kiwanda cha nguo cha urafiki kinachojulikana Kama “Tanzania-China Friendship Textiles Company” kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam ambalo ni dola milioni 15 sawa na Sh34.7 bilioni.
Hii si mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kuwaomba wakopeshaji wa kimataifa kusamehe madeni. Aprili mwaka jana aliwaomba wakopeshaji wa kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia kuzisamehe nchi za Afrika madeni ili fedha hizo ziende kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).
Soma zaidi:
- Wawekezaji kutoka China kuyaongezea thamani madini ya Tanzania
- Serikali yajiwekea mikakati kuongeza mapato ya utalii kutoka China
Aidha, Rais Magufuli ameiomba China isaidie Tanzania katika miradi mitatu mikubwa ya umeme wa maji ya mkoani Njombe ya Lumakali na Luhuji pamoja na ujenzi wa kilomita 148 za barabara visiwani Zanzibar.
Mbali na miradi hiyo, Rais Magufuli ameiomba China kama itawezekana iweze kutoa mkopo hata wa masharti nafuu kufanikisha ujenzi wa kipande cha reli kutoka Isaka hadi Makutopora mkoani Dodoma.
Nchi hizo mbili zimekuwa zikishirikiana katika mambo mengi ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Yi alikuwa katika ziara ya siku mbili nchini ikiwa ni moja ya nchi anazozitembelea safari katika bara la Afrika.
Yi amesema China itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuendelea kudumisha uhusiano uliodumu kwa muda mrefu.
Amesema atafikisha maombi ya Rais Magufuli kwa mwenzake wa China, Xi Jinping ili yafanyiwe kazi huku akiyataka makampuni ya China yaliyopo Tanzania kufanya kazi kwa weledi.
“Nachukua fursa hii kuyaagiza makampuni ya China yanayotekeleza miradi hapa nchini Tanzania kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia kwanza maslahi ya Tanzania,” amesema Yi.