November 24, 2024

Kupiga chafya siyo dalili ya Corona

WHO yasema siyo miongoni mwa dalili za ugonjwa huo, lakini maji maji ya chafya yanaweza kusababisha COVID-19.

  • WHO yasema siyo miongoni mwa dalili za ugonjwa huo.
  • Lakini maji maji ya chafya yanaweza kusababisha COVID-19.
  • Uvaaji wa barakoa na kutumia tishu kunaweza kuwakinga watu.

Dar es Salaam. Kupiga chafya imekuwa ni dalili ambayo mara nyingi inahusishwa na watu wanaopata mafua ya kawaida (flu) lakini wapo baadhi ya watu wanaohusianisha jambo hilo la kiafya na ugonjwa wa corona. 

Watu wanaohusiana chafya na corona wanaamini kuwa kupiga chafya ni moja ya dalili kuu ya mtu mwenye ugonjwa wa Corona, dhana ambayo siyo sahihi kwa mujibu wa taasisi mbalimbali za afya ulimwenguni.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC), kupiga chafya siyo dalili inayoweza kumtambulisha mtu kuwa ana virusi vya COVID-19. 

CDC inaeleza kuwa kupiga chafya inaweza kuwa ni ishara kuwa vumbi, uchafu au bakteria wameshambulia mfumo wa upumuaji.


Zinazohusiana:


Hata katika orodha ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya dalili za watu wenye Corona, kupiga chafya haijaorodheshwa kama moja ya dalili za watu waliopata virusi hivyo. 

WHO imeeleza kuwa dalili za Corona ni homa kali na kujihisi kuchoka, kukohoa, kupata shida ya kupumua, kuuma kwa misuli na kukosa uwezo kunusa harufu na ladha. Dalili hizo hazijabadilika hata baada ya aina mpya ya kirusi cha corona kubainika siku za hivi karibuni barani Ulaya.

Dalili hizo hujionyesha kwa mtu kati ya siku mbili hadi 14. 

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa maji maji yanayotokana na kupiga chafya yanaweza kusambaza virusi na ndiyo maana unashauriwa kutumia tishu wakati wa kitendo hicho.

Tahadhari nyingine ni kuosha mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuvaa barokoa. 

Ni muhimu kupata taarifa za uhakika kuhusu Corona kutoka kwa mamlaka za afya zinazotambulika kisheria ili kuepuka madhara ya habari za uzushi kuhusu ugonjwa huo.