November 24, 2024

Wananchi watakavyonufaika bandari mpya Kigoma

Ni Bandari ya Kagunga iliyopo Wilaya ya Kigoma ambayo ni kiungo cha biashara na usafirishaji mizigo.

  • Ni Bandari ya Kagunga iliyopo Wilaya ya Kigoma.
  • Ilikalimilika tangu 2017, Serikali yaamuru ianze kutumika Januari 1, 2021.
  • Itaongeza kasi ya biashara na usafirishaji wa mizigo mkoani Kigoma. 

Dar es Salaam. Huenda wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakaanza wakanufaika na shughuli za kibiashara, baada ya Serikali kuagiza soko na Bandari ya Kagunga mkoani humo kuanza kutoa huduma Januari mosi mwaka ujao. 

Bandari hiyo iliyopo Wilaya ya Kigoma itakua ni kiungo muhimu cha shughuli za biashara na usafirishaji katika Ziwa Tanganyika na nchi jirani ikiwemo Burundi. 

Waziri Mkuu Kassim Majali amesema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ulikamilika mwaka 2017 ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu kwa gharama ya Sh3.8 bilioni.

Hata hivyo, mpaka sasa bandari hiyo haijaanza kutumika, jambo linalowakosesha wananchi fursa za mbalimbali za kukua kiuchumi.

“Leo nimekuja hapa kuona bandari, hii bandari ilikamilika mwaka 2017 imekaa tu, nyumba zimejaa popo tu na mle ndani kumejaa takataka na mmefagia jana baada ya kusikia mimi nakuja.

“Hovyo kabisa nawauliza hapa wanajikanyaga tu tuna mtumishi hapa hakuna mtumishi amekuja jana badaa ya kusikia nakuja hovyo kabisa hawa,” amesema Majaliwa Desemba 18, 2020 alipotembelea bandari hiyo. 


Soma zaidi: 


Aidha, Majaliwa ameipa wiki mbili kuanzia jana Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe kwamba ifikapo Januari Mosi mwakani bandari hiyo ya kimkakati iliyoko katika kata ya Kagunga iwe imeanza kutoa huduma.

“…tarehe moja ya mwezi wa kwanza mwaka 2021 nataka bandari hii ianze kazi, nenda mkajipange. Hapa hakuna mtumishi hamisha watumishi kama wapo Dar es Salaam, kama wapo Kigoma leta watumishi hapa wawatumikie wananchi kwenye bandari hii,” amesisitiza Mjaliwa. 

TPA wametakiwa kuruhusu meli na boti za watu binafsi kufanya kazi ya kutoa huduma katika bandari hiyo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa urahisi. 

Pia ameagiza soko la kisasa la Kagunga nalo lianze kazi siku hiyo hiyo ili kuwawezesha wananchi kufanya biashara na kuinua kipato chao.