Barua ya wazi ya afya kuelekea mwisho wa mwaka 2020
Usiache kuipenda afya yako ya akili. Jiepushe na msongo usio wa lazima. Usijiweke upweke na usiruhusu kuishi na vitu vingi akilini mwako. Fanya kila kitu kwa hatua.
- Nina imani umeshaandaa mipango kwa ajili ya mwaka mpya ujao.
- Umekumbuka kuweka mipango ya afya pia?
Habari rafiki, u hali gani? Natumaini barua hii itakukuta ukiwa buheri wa afya katika utimamu na utimilifu wake. Lakini iwapo itakukuta katika changamoto na adha za magonjwa basi dua zangu ni kwamba ukapate nafuu na uponyaji wa haraka.
Rafiki mpendwa, mwaka ndiyo huu unaelekea ukingoni. Nami nikaona walau tukumbushane na kuelekezana vitu kadhaa vya kiafya tunapoelekea kumaliza mwaka na kuanza mwaka mwingine wa 2021.
Rafiki, niliwahi kukukumbusha kuhusu bima ya afya na umuhimu wake katika kukusaidia wewe kupata matibabu kwa urahisi. Ulifuatilia hilo rafiki? Ugonjwa hauna hodi. Huja pale usipodhani. Lakini pia huweza kuwakumba ndugu na watu wako wa karibu.
Gharama za matibabu huwa ni mzigo mkubwa. Rafiki, nakusihi tena kwamba iwapo hujapata bima ya afya, usifanye ajizi, anza kufuatilia taratibu za bima. Tunapoenda kuanza mwaka mpya basi uwe na bima yako mkononi tayari kwa kupata huduma bora.
Pia niliwahi kukuandikia kuhusu utaratibu wa kupima afya yako na kwamba walau mara tatu kwa mwaka ufike kufanya ‘check-up’ ya jumla ya mwili wako. Hii itakusaidia wewe kuzijua dalili hatarishi za magonjwa kabla hayajawa sugu. Umefanya hivyo rafiki? Kama bado unangoja nini?
Katika muda uliobaki tafuta muda wako uende hospitali na kufanya uchunguzi wa kiafya ili uanze mwaka na uthabiti wa afya.
Nadhani unakumbuka dodoso langu nilikupatia kuhusu chaguzi za mtindo sahihi wa maisha ambao unachochea utimamu wa afya ya mwili. Nilikugusia namna chakula kilicho bora na chenye mpangilio ni dawa tosha kwa ajili ya mwili wako.
Lakini sikuishia hapo nilikueleza kuwa kupunguza vyakula vya mafuta na kuzingatia uzito na kufanya mazoezi kutakusaidia wewe kuepukana na magonjwa nyemelezi ikiwemo magonjwa ya moyo. Rafiki, ijali afya yako.
Zinazohusiana:
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa
- Tahadhari za kuchukua kuepuka uume kuvunjika
Yakupasayo kufanya
Nina imani ya kwamba umeshaandaa mipango kwa ajili ya mwaka mpya ujao. Lakini umekumbuka kuweka mipango ya afya pia? Mipango ya afya ni muhimu. Afya yako ikiwa sawa itaakisi na kuchochea utimizwaji wa malengo yako. Lakini afya yako isipokua timamu basi malengo yako hayatotimia.
Weka mpango mkakati wa kupata chanjo muhimu kama chanjo ya homa ya ini, iwapo una mpango wa kuanzisha familia, fuatilia kuhusu afya ya uzazi kabla ya kupata mtoto. Jiwekee mipango ya kuimarisha afya kwa kufanya vipimo muhimu. Pangilia milo yako, mazoezi na kazi. Zingatia kila ufanyalo.
Usiache kuipenda afya yako ya akili. Jiepushe na msongo usio wa lazima. Usijiweke upweke na usiruhusu kuishi na vitu vingi akilini mwako. Fanya kila kitu kwa hatua. Pangilia mtriririko wa kazi zako ili kuondoa mrundikano.
Rafiki, kukunjwa kwa jamvi si mwisho wa maongezi, sitaki kukuchosha kwa maneno mengi. Barua hii ikukute ukiwa buheri wa afya na ikukumbushe kwamba rafiki yako ninakujali sana. Nakutakia Sikukuu njema za Krismas na Heri ya Mwaka Mpya wa 2021.
Kama kawaida, nipo!!
Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.