November 24, 2024

Gharama utakazolipa unapoamua kujichubua ngozi-3

Ngozi yako bado ni nzuri haihitaji kubadilishwa bali kutunza vizuri na bado ukavutia na kupata urembo unaoutaka.

  • Paka mafuta yanayoendana na hali ya hewa ya eneo lako.
  • Kabla ya kutumia mafuta, tafuta ushauri wa wataalam ili kufahamu kama yatakufaa. 
  • Pia tathmin sabuni na bidhaa zingine za kuosha mwili unazotumia. 

Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu ambao wako katika mpango wa kuianza safari ya kubadilisha rangi ya ngozi yako kwa kufikiri utapata muonekano mzuri wa sura. Umedanganyika!

Ngozi yako bado ni nzuri haihitaji kubadilishwa bali kutunza vizuri na bado ukavutia na kupata urembo unaoutaka. 

Ili kuepukana na madhara yatokanayo na kujichubua ikiwemo kuharibika kwa ngozi na kupoteza muonekano wako wa asili, zingatia mambo haya:

Tumia mafuta ya kawaida yasiyo na kemikali nyingi

Jessica Kimoso ni mmoja wa wadau wa urembo na ajabu ni kuwa, hatumii pesa nyingi kununua vipodozi kwa ajili ya ngozi yake mbali na mafuta ya mgando aina ya Vaseline.

Jessica ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema, yeye anafahamu kuwa kiwango cha mafuta kwenye ngozi yake ni cha wastani hivyo kwa ngozi yake amechagua kutumia mafuta hayo na hakumbuki kuwahi kutumia mafuta aina nyingine.

Bini huyo amesema anayapenda kwa sababu yanapatikana kwa urahisi na “yametengenezwa bila kuwekewa kemikali nyingi”.

Chagua mafuta asilia yanayoendana na aina ya ngozi yako

Kwa wale ambao ngozi zao hazipatani na mafuta yenye kemikali za viwandani, bado wana nafasi ya kuzing’arisha ngozi zao kwa kupata mafuta ya asili. 

Mafuta hayo ambayo ni rahisi kupatikana yanatokana na miti ni pamoja na mafuta ya nazi, alizeti, mnyonyo na mzeituni.

Mwanasheria kutoka jijini Dar es Salaam Neema Kibodya ameiambia Nukta (www.nukta) kuwa yeye anatumia mafuta ya nazi ambayo yamemfanya kuwa mrembo kuliko hata wanawake wengine wanaobadilisha mafuta mara kwa mara. 

“Usoni kinachopita ni sabuni, maji basi, mafuta ni sehemu zingine za mwili,” anasema Kibodya ambaye anaamini kila ngozi ni nzuri lakini ili iwe na muonekano mzuri ni vyema muhusika apake mafuta yanayomfaa. 

Licha ya kuwa unatakiwa kuzingatia mafuta unayopaka kwa ajili ya ngozi yako lakini kufahamu aina ya sabuni unayotumia ni muhimu zaidi ili kujiweka salama. Picha| Neema Kafwimi.

Hali ya hewa huathiri ngozi

Wakati mwingine baadhi ya watu hawafahamu kuwa hali ya hewa ya eneo fulani huathiri afya ya ngozi na njia pekee ni kupaka mafuta yanayoendana na mabadiliko hayo kuliko kukimbilia kujichubua. 

Mathalan, kwa watu wanaoishi katika maeneo yenye baridi wanahitaji mafuta mazito yakiwemo ya mgando kwa sababu yanatoa kinga kwa ngozi ikilinganishwa na watu wanaoishi kwenye joto ambako mafuta mepesi (yenye asili ya maji maji) yanaweza kuwafaa. 

Evon Evance ambaye ni mdau wa masuala ya ubunifu anasema ngozi za kila mtu huwa na mahitaji tofauti kulingana na hali ya hewa, hivyo ni jukumu la mhusika kutambua hilo na kulifanyia kazi. 

Soma maelezo ya mafuta kabla ya kununua

Mratibu mradi wa D-Tree International, Neema Kafwimi ameshauri watu kuwa makini kwa kusoma bidhaa wanazonunua kwa ajili ya ngozi zao.

“Ukiona neno gumu na haulielewi, uliza wataalamu watakupatia maana yake. Ni muhimu kufanya utafiti kabla ya kuamua kutumia aina fulani ya kipodozi,” ameshauri Kafwimi.


Soma zaidi:


Kuwa makini na sabuni unayonunua

Licha ya kuwa unatakiwa kuzingatia mafuta unayopaka kwa ajili ya ngozi yako lakini kufahamu aina ya sabuni unayotumia ni muhimu zaidi ili kujiweka salama. 

Mtaalam wa bidhaa asilia za nywele na ngozi, Rachel Essau anasema kabla ya watu kutumia sababuni wanapaswa kusoma maelezo yake kama yanaendana na ngozi zao.

“Kuna sabuni ambazo mimi nikizitumia ninakuwa sawa lakini wengine wakizitumia wanapata muwasho na hata chunusi,” anasema Essau.

Kwa ambao wameathirika na kutumia vipodozi vya kujichubua, Essau amewashauri kutumia bidhaa za asili ukiwemo unga wa liwa, asali na manjano.

“Mtu anaweza kununua unga wa manjano akachanganya na maji kidogo akapaka usoni na kisha kusubiri kwa muda kidogo kabla ya kuosha uso wake,” anasema Essau.

Mwanadada huyo anabainisha kuwa watu walioathirika na kujichubua waachane na vipodozi vinavyoathiri ngozi zao na kutafuta ushauri kwa watalaam wa ngozi. 

Ngozi yako ni nzuri ithamini, ipende na itunze, usitumie njia zisizo halali za kujichubua kutafuta urembo ambao unaweza kugharimu maisha yako.