Gharama utakazolipa unapoamua kujichubua ngozi-1
Kati ya gharama hizo ni kujiingiza katika hatari za kiafya zinazoweza kusababisha kifo.
- Kati ya gharama hizo ni kujiingiza katika hatari za kiafya zinazoweza kusababisha kifo.
- Wadau wa urembo wanahusisha kujichubua na watu kujiona duni na historia ya utawala wa wakoloni barani Afrika.
- Kemikali zinazotumika kujichubua ni chanzo cha kuingiza sumu mwilini.
Dar es Salaam. Kila kitu kizuri kina gharama ambayo mtu anayetaka kukipata anatakiwa kuilipa. Gharama inaweza kuwa fedha, muda au vitu.
Baadhi ya gharama ambazo mtu analipa humuweka katika hatari ya kupata athari za kiafya na hata kifo.
Kutafuta urembo au muonekano mzuri wa sura ni miongoni mwa vitu ambavyo wanawake na wanaume huwekeza nguvu zao na hata wengine kutumia njia zisizo sahihi kufikia kuupata.
“Nilikuwa nabezwa sana na rangi yangu. Mtu angesema amerekodi video lakini hata sionekani. Kazi zangu zenyewe ni usiku nikawa nashindwa kukuza brandi yangu vizuri. Sikuwa na namna zaidi ya kujing’arisha kidogo,” anasema John (jina siyo halisi).
John ambaye ni mwanamuziki anayetumbuiza kwenye kumbi za muziki jijini Dar es Salaam anasema kwa sasa ana muonekano mzuri wa rangi nyeupe na anajisikia amani.
Hata hivyo, kijana huyo ambaye alijichibua takriban miaka miwili iliyopita, ameanza kupata madhara ya urembo wake baada ya ngozi yake kutostahimili jua kutokana na kuwa nyepesi na laini.
“Ninalazimika kwa sasa kununua mafuta maalum kwa ajili ya kuikinga ngozi yangu na jua kali. Saa zingie naweza kukaa ndani siku nzima,” anasema John wakati akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Baadhi ya wanaojichubua hushindwa kufikia taswira za muonekano waliokuwa nayo. Picha| EATV.
John ni miongoni mwa Watanzania wengi ambao wamepata na wanaendelea kupata madhara mbalimbali ikiwemo ya kiafya kutokana na kutumia vipodozi kubadili ngozi zao (skin bleaching).
Baadhi ya njia zinazotumika kujichubua ni pamoja na matumizi ya mafuta, dawa za kung’arisha ngozi, vidonge (tembe), sindano na wengine hutumia mkorogo ikiwemo bidhaa za usafi.
Kujichubua ni zaidi ya urembo na muonekano mzuri
Suala la watu kubadili ngozi zao ili ziwe nyeupe ni matokeo ya sababu mbalimbali ambazo ni zaidi ya urembo ambao baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha nao.
Mdau wa masuala ya urembo jijini Dar es Salaam, Charlotte Nzuki anasema kujichubua kuna uhusiano mkubwa na mtazamo ambao wakoloni walioujenga katika fikra za Waafrika kuwa ngozi nyeusi haina thamani hasa katika urembo.
“Tulilazimishwa kuamini kuwa rangi nyeusi kwenye ngozi zetu haifikii viwango vya urembo au mtu anapokuwa na rangi nyeusi hajawa mwanadamu aliyekamilika,” anasema Nzuki.
Soma zaidi:
- Sababu za wanawake wa Tanzania kurudia nywele za asili
- Unayopaswa kuzingatia kabla ya kufanyiwa “massage”
- Tahadhari za kuchukua kuepuka uume kuvunjika
Mwanadada huyo anabainisha kuwa hata baada ya ukoloni, vyombo vya habari yalitoa kipaumbele katika kuonyesha kuwa ngozi nyeupe ndiyo urembo kwa kutumia matangazo ya bidhaa na huduma.
“Hilo pia lina mchango mkubwa wa kuwafanya watu wajichubue. Mathalani, kwa baadhi ya makabila wanathamini zaidi mwanamke ambaye ni mweupe na hata mahali yao ilikuwa juu zaidi kuliko dada zao wenye ngozi nyeusi,” anaeleza Nzuki.
Hata hivyo, wengine hujichubua kwa kufuata mkumbo au kujiona duni kifikra (inferiority complex) na kutaka kuwa kama watu weupe ili kufikia viwango fulani wanavyofikiri kuwa ni vya kibinadamu.
“Watu wanadanganyana. Wapo ambao wanameza vidonge na unavyosema mabaka meusi wala huwezi kuyaona. Hao unaowaona ni wenye mikorogo ambao baadhi yao wanaweka hadi jiki.
“Wataringa na kutesa saa hizi lakini fainali ni uzeeni. Uzuri ni ule ambao unazaliwa nao na unatakiwa ujikubali. Mimi ni mweusi na najua ngozi yangu ina thamani,” anasema Gladness Michael, mjasiriamali wa vipodozi jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau wa urembo wahusianisha kujichubua na ukoloni. Picha| JamiiForums.
Kilichojificha nyuma ya vipodozi za kujichubua
Vipodozi vinavyotumika kujichubua vina kemikali ambazo huingilia mfumo wa homoni zinazosimamia ustawi wa ngozi ya mwili.
Wataalam wa afya ya ngozi wanaeleza kuwa kemikali hizo siyo salama kwa ngozi ya binadamu na zina madhara makubwa ya kiafya, endapo watumiaji hawatazingatia ushauri wa kitaalam kabla ya kutumia.
“Kikubwa cha kuangalia ni nini unalisha kwenye mwili wako baadhi ya vipodozi vinawekewa Aluminium na Mercury (kemikali za aluminiamu na zebaki) vitu hivi sio vizuri kwa mwili wako,” anasema Dk Elizabeth Lema kutoka kliniki ya tiba asili ya Cornwell Naturopathic Clinic iliyopo jijini Dar es Salaam.
Katika makala inayofuata tutaangazia madhara ya kujichubua kiafya, kiuchumi na njia za zitakazokusaidia kurejesha ngozi yako ya asili.