October 6, 2024

Kicheko kwa wamiliki wa vyombo vya moto wakifunga mwaka 2020

Baada ya bei za mafuta kwa mwezi Desemba kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi uliopita zikichangiwa na kuporomoka kwa bei ya nishati katika soko la dunia.

  • Bei ya petroli na dizeli yashuka kwa viwango tofauti. 
  • Wakazi wa jiji la Dar es Salaam watanunua petroli kwa Sh1,865 kwa lita, dizeli (Sh1,687).
  • Ahueni ya kushuka kwa bei ya mafuta itawashukia pia wakazi wanaohudumiwa na bandari za Mtwara na Tanga. 

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto huenda wakafunga mwaka 2020 kwa kicheko, baada ya bei za mafuta kwa mwezi Desemba kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi uliopita zikichangiwa na kuporomoka kwa bei ya nishati katika soko la dunia.

Bei mpya kikomo kwa mwezi Desemba zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) zinabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh37 kwa lita huku ile ya dizeli ikipungua kwa Sh47 kwa lita.

Ahueni hiyo imeenda hadi katika mafuta ya taa ambayo bei yake imeshuka kwa Sh86 kwa lita.

Hiyo itawafanya wakazi wa jiji hilo la kibiashara kununua petroli kwa Sh1,865 kwa lita, dizeli (Sh1,687) na mafuta ya taa kwa Sh1,621.

Mbali na mafuta yaliyoingizwa kupitia Dar es Salaam, bei ya mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari za Mtwara na Tanga nazo zimeshuka, jambo linalowaokoa pia wakazi wa maeneo hayo kutoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hizo muhimu kwa ajili ya usafiri, viwanda na nishati.

Ewura inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imepungua kwa Sh107 kwa lita na dizeli imeshuka kwa Sh27 kwa lita.

Hata hivyo, bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa Novemba 4, 2020. 

“Hii ni kwa sababu, kwa mwezi Novemba 2020 hakuna shehena ya Mafuta ya Taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” amesema Kaimu Mtendaji Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje katika taarifa yake iliyotolewa Desemba 1. 

Mafuta hayo hutumiwa na wakazi wa mikoa ya Kaskazini mwa nchi ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, na Manyara.


Soma zaidi:


Nao Wakazi wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wao nao watashuhudia punguzo la bei za rejareja kwa petroli na dizeli huku bei ya  mafuta ya taa ikibaki ile iliyotumika mwezi uliopita.

Bei kikomo ya rejareja kwa petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Mtwara inayotumiwa na mikoa hiyo ya kusini  imeporomoka kwa Sh70 kwa lita huku dizeli nayo ikipungua kwa Sh4 kwa lita.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” amesema Chibulunje. 

Taarifa ya Ewura imeeleza kuwa bei hizo mpya zinaanza kutumika kuanzia kesho Novemba 2, 2020 nchini kote.

Wakazi wa Uvinza (Lugufu) wao ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko wote nchini ikiwa ni Sh2,109 na dizeli kwa Sh1,930  kwa lita kutokana na gharama mbalimbali zikiwemo za usafiri.