October 7, 2024

Madhara yatakayokupata usipotibu ugonjwa mapema

Ni pamoja na kutumia gharama kubwa za matibabu na kufariki dunia.

  • Ni pamoja na kutumia gharama kubwa za matibabu.
  • Pia ugonjwa kukosa tiba kabisa na hatimaye kifo.
  • Ukipata maumivu ya mwili, nenda hospitali kapate tiba. 

Nabaki na tafakuri nzito, wakati nikipitia baadhi ya taarifa za wagonjwa wangu kwenye mafaili kadhaa katika kabati ya kutunzia kumbukumbu za wagonjwa katika kituo cha kazi.

Tafakuru hiyo inakuja kwa sababu nakutana na rekodi za baadhi ya wagonjwa zisizofurahisha hasa za wagonjwa ambao nina ukaribu nao. 

Taarifa zao ambazo zipo kwenye mafaili ya hospitali hazifurahishi. Kimsingi hakuna kinachofurahisha kuhusu ugonjwa, lakini vipo vile ambavyo husikitisha zaidi kuliko vingine. 

Rekodi za mafaili yao zinaonyesha wamefikia hatua mbaya za ugonjwa na wako katika hatari kugharimika zaidi kupata tiba. 

Changamoto kubwa ya kiafya inyowapata watu ni kufika hospitali katika hatua za mwisho au sugu za ugonjwa. Katika hatua hizi, ugonjwa unakua umefika katika hatua mbaya isiyoweza kurejesha hali ya kawaida.

Wakati mwingine mgonjwa hutumia gharama kubwa au kupoteza baadhi ya viungo vya mwili na hata kufariki dunia.


Zinazohusiana:


Utambuzi wa dalili za ugonjwa unapofanyika mapema huwezesha utolewaji wa tiba husika mapema, kwa namna hiyo humsaidia mgonjwa kupona na kurudia hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. 

Unapohisi dalili za ugonjwa ama unapojisikia vibaya na hali hiyo ikajirudia mara kadhaa, ni vyema kufika hospitali na kuonana na mtoa tiba ili uweze kuhudumiwa ipasavyo. 

Matumizi ya dawa za kuondoa maumivu mara kwa mara kwa tatizo ambalo halijatambuliwa na mtaalamu ni hatari. Maumivu ni ishara ambayo mwili hutumia kutoa taarifa za hitilafu sehemu fulani. 

Usipuuzie maumivu, uvimbe au hali yoyote isiyo ya kawaida kwa muda mrefu. Muone muhudumu wa afya akuhudumie.

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.