Jamii ishikamane kutokomeza ukatili wa kijinsia Tanzania
Elimu na majadiliano yatasaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
- Idadi ya vitendo vya ukatili vinavyoripotiwa yaongezeka,
- Jamii yatakiwa kuimarisha nguvu kutokomeza vitendo hivyo.
- Polisi yashauriwa kuongeza kasi ya upelelezi wa kesi za ukatili.
Mwanza. “Ni takribani miaka 15 nimeishi maisha ya kupigwa, kutukanwa na manyanyaso ya kila aina, kitendo ambacho kiliharibu maisha yangu na familia yangu ambayo hatukuweza kufanya maendeleo,” Marry Jackson, mkazi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Mama huyo wa watoto sita anasimulia jinsi alivyokua anafanyiwa ukatili wa kijinsia na mume wake, jambo lililozorotesha maendeleo ya familia yake.
Hata hivyo, mambo yamebadilika, amani imerejea katika familia ya Marry ambapo suala la kupigwa na kuteswa na mume wake halipo tena baada ya wawili hao kupata msaada wa kisheria na ushauri wa masuala ya usawa wa kijinsia.
Marry anaungana na wanawake wengine duniani katika kampeni maalum ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mkoani Mwanza, ambayo inalenga kuijengea uwezo jamii kutambua umuhimu wa usawa wa kijinsia na kusimama kupinga ukatili wa aina zote hasa unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto.
Takwimu za kitengo cha dawati la jinsia cha Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza zinaeleza kuwa kesi 1,387 za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto zimeripotiwa katika kitengo hicho kati ya mwezi Januari hadi Oktoba 30 mwaka huu.
Kati ya kesi hizo, 455 zimefikishwa mahakamani huku zingine 661 zikiwa katika hatua mbalimbali za upelelezi.
Pamoja na mafanikio ya kuripotiwa kwa kesi hizo bado kuna changamoto ya kuchelewa kwa kesi hizo kufika kwa wakati mahakamani na baadhi ya wafungua mashtaka kushindwa kuendeleza kesi hizo na hivyo kusuluhisha nyumbani.
Zinazohusiana:
- Uongozi, ardhi kuwatoa kimaisha wanawake vijijini
- Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyekua akizungumza Novemba 25, 2020 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia Mwanza ameliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua madhubuti kumaliza tatizo hilo ili kuwapatia haki wahanga wa vitendo vya ukatili.
Anasema mikoa ya Kanda ya Ziwa inatajwa kuongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia Tanzania, hivyo kuna haja ya kila mtu kutimiza wajibu wake kukabiliana na vitendo hivyo.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupinga ukatili wa kijinsia, bado wadau wa masuala ya usawa wana kazi kubwa ya kutoa elimu na kuwalinda wanawake na watoto, ikizingatiwa kuwa baadhi ya vitendo hivyo viovu haviripotiwi kwenye mamlaka husika.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto la Kivulini, Yassin Ally amewataka wazazi kuwalinda na kuwaelimisha watoto kuhusu ukatili wa kijinsia ili kujenga jamii yenye usawa.
Amesema njia nyingine ya kumaliza tatizo hilo ni jamii kuzungumza kwa uwazi juu ya tatizo hilo kwa majadiliano, midahalo na mikutano ya wadu mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi na wananchi.
Novemba 25 kila mwaka ni siku ya kwanza ya kampeni ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kilele chake ni Desemba 10, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu,
Kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni wakati wa kutafakari juu ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.