November 24, 2024

Walichokisema wagombea urais baada ya kupiga kura Tanzania

Wawataka Watanzania kudumisha amani na utulivu wakati wakitimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo

  • Rais John Magufuli awataka Watanzania kudumisha amani na upendo.
  • Mgombea wa Chaumma, Hashim Rungwe amewahimiza watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura. 
  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itaanza kutangaza matokeo ya urais leo usiku.

Dar es Salaam. Baadhi ya wagombea wa urais Tanzania akiwemo Rais John Magufuli wamepiga kura huku wakiwataka Watanzania kudumisha amani na utulivu wakati wakitimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Uchaguzi Mkuu unaofanyika leo (Oktoba 28, 2020) ni mahususi kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani na Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Magufuli akiambatana na mkewe Mama Janet Magufuli tayari wamepiga kura Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. 

“Mimi nimeshapiga kura na mke wangu ameshapiga kura, kwa hiyo tumetimiza wajibu wetu wa kuchagua,” amesema Rais Magufuli baada ya kupiga kura. 

Amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura huku akiwahimiza kudumisha amani na utulivu kipindi hiki cha uchaguzi.

“Wito wangu kwa Watanzania tujitokeze kwa wingi kupiga kura, twende tukapige kura ambayo kila mmoja atakuwa nayo katika moyo wake. 

“Nipende kusisitiza, amani lazima tuendelee kuitunza kama Taifa kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi,” amesema Magufuli. 

Katika uchaguzi wa mwaka huu, wapiga kura milioni 29.18 wenye sifa wamejiandiisha katika daftari la wapiga kura kutoka milioni 23.16 waliojiandikisha mwaka 2015.

Zoezi la upigaji kura likiendelea katika maeneo mbalimbali Tanzania. Picha|Mtandao.

Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema mwenendo wa upigaji kura kwa baadhi ya vituo visiwani humo alivyopita ni mzuri. 

Maalim Seif aliyepiga kura katika Kituo cha Garagara Mjini Magharibi katika kisiwa cha Unguja, amewataka watu kujitokeza na kutimiza wajibu wao. 

Naye Mgombea wa kiti cha urais chama cha Chaumma, Hashim Rungwe amesema wananchi waliojitokeza kupiga kura ni wachache hivyo amewaomba wajitokeze kwa wingi kwani kupiga kura ni haki yao ya msingi.

“Watu nafikiri siyo wachache sana au wengi, naomba wananchi waje wapige kura,” amesema Rungwe wakati akihojiwa na gazeti la Mwananchi jijini Dar es Salaam. 

Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha UPDP, Twalib Kadege naye amepiga kura yake akiwa mkoani Mbeya licha ya kuwa alikuwa hana kitambulisho cha mpiga kura kwa sababu alikisahau jijini Dar es Salaam na aliomba atumie kitambulisho cha Taifa. 

Akihojiwa na gazeti la Mwananchi, Kadege amesema ameridhishwa na mwenendo wa upigaji kura na amewataka wananchi kufanya hivyo kabla zoezi halijafungwa hapo baadaye. 

Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa saa 10 jioni ili kupisha zoezi la kuhesabu kura na taratibu za kuwatangaza washindi chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan aliyepiga kura katika kituo cha SOS Mombasa Zanzibar amewasihi watu waliopo nyumbani na wanahofia usalama wao wajitokeze kupiga kura kwasababu kila kitu kipo vizuri na zoezi linakwenda haraka. 


Soma zaidi: 


Utaratibu wa kutoa matokeo

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Wilson Mahera amesema kuanzia leo usiku Jumatano Oktoba 28, 2020 tume hiyo itaanza kutangaza matokeo ya kura za urais kutoka kwenye majimbo mbalimbali ya uchaguzi kadiri watakavyokuwa wanapokea na litaendelea mpaka kesho. 

Amesema katika maeneo aliyotembelea jijini Dar es Salaam zoezi la upigaji kura linaendelea vizuri huku akiwataka wasimamizi wa vituo kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wazee, wajawazito  na walemavu. 

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa sita tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1995. 

Wakati ukitimiza wajibu wako wa kupiga kura, zingatia mambo hayo ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.