October 6, 2024

App inayowahakikishia hedhi salama wanawake Tanzania

App hiyo inawawezesha wanawake kuongea na wataalamu wa afya kuhusu masuala ya uzazi wakati wowote.

  • Ni app ya kwanza inayotumia lugha ya Kiswahili kuwasaidia wanawake wanaopata changamoto ya kuhesabu siku zao. 
  • Pia inatoa elimu ya uzazi kupitia madaktari bingwa wa masuala ya wanawake. 
  • Baadhi ya wanawake wamesema itawapunguzia aibu wanayopata wakati wa hedhi. 

Dar es Salaam. Kama wewe ni mwanamke na umekuwa ukipata changamoto ya kufuatilia mzunguko wa hedhi kila mwezi, sasa una kila sababu ya kutabasamu kwa sababu teknolojia imekuletea suluhisho. 

Changamoto hiyo huwaletea msongo wa mawazo wanawake hasa pale wanapopata mimba zisizo tarajiwa au kujichafua. 

Lakini simu janja inaweza kufanya kila kitu kuifanya hedhi yako ikupe thamani na fahari ya kuwa mwanamke. 

Kiwanda cha kuingiza bidhaa za hedhi cha AnuFlo kilichopo jijini Dar es Salaam kimezindua programu tumishi ya simu (app) ya kwanza ya Kiswahili ya  “Hedhi” ambayo inalenga kutatua changamoto za hedhi kwa wanawake zikiwemo kuhesahau siku zao za hedhi.

Pia app hiyo ambayo imepakuliwa na watu zaidi ya 100, inawawezesha wanawake kuongea na wataalamu wa afya kuhusu masuala ya uzazi wakati wowote.

Flora Njelekela, Mkurugenzi Mkuu wa AnuFlo Industries Ltd akiongea wakati wa uzinduzi wa Hedhi App jijini Dar es Salaam. Picha| AnuFlo.

Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Flora Njelekela amesema app hiyo itawasaidia wanawake kufahamu mabadiliko yatakayojitokeza katika mzunguko wa hedhi na kukabiliana na mihemko ya mwili inavyoathiri afya zao. 

“Kwa mujibu wa tafiti zetu, tumegundua kwamba mabinti wengi wanapata mimba zisizotarajiwa kutokana na kukosa taarifa sahihi juu ya mzunguko wa hedhi. Ujio wa app hii ya Hedhi utawasaidia kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi na kudhibiti mimba zisizotarajiwa,” amesema Njelekela.

Mkurugenzi wa AnuFlo Industries Ltd Flora Njelekela akiongea wakati wa uzinduzi wa Hedhi App jijini Dar es Salaam. Picha| AnuFlo.

Kwanini app hiyo?

Baadhi ya watu huenda wanajiuliza kwa nini usaidiwe kukumbuka siku zako wakati unaweza kuzihesabu mwenyewe. Jibu ni kuwa “siri ya mtungi aijuaye kata.”

App hiyo itawasaidia wanawake kama mfanyabiashara jijini Dar es Salaam, Charlotte Nzuki ambao wanapata changamoto ya kuhesabu siku zao kwa kukariri kichwani. Ili kujiweka salama wanahitaji usaidizi wa teknolojia. 

“Mimi naishukuru sana teknolojia kwasababu inasaidia kufuatilia hedhi kwa ukaribu. Apps za kuangalia mwenendo wa hedhi haziishii kuangalia mwenendo wa hedhi pekee, zipo ambazo zinakumbusha hadi kumeza dawa kama unaumwa,” amesema Nzuki ambaye anatumia apps hizo kwa zaidi ya miaka mitano.

Naye Mjasiriamali kutoka jijini Arusha Florance Shirima amesema kuhesabu siku kila mwezi inachosha na mtu yeyote anaweza kusahau. Hivyo uwepo wa teknolojia unakuwa na umuhimu ili kuepuka kupata mimba. 

“Muda pekee ninapokuwa makini kuhesabu siku zangu ni pale ninapokuwa kwenye mahusiano kwa sababu najua nitakuwa ninajamiiana. Mbali na hapo sitilii maanani,” amesema Shirima.

Hivyo ni sawa kusema, apps ambazo zinamkumbusha mwanamke au msichana juu ya mzunguko wa hedhi zake, zina mchango mkubwa katika kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), wasichana 20,000 wenye umri chini ya miaka 18 katika nchi zinazoendelea hujifungua kila siku sawa na vizazi milioni 7.3 kwa mwaka kutokana na kukosa taarifa sahihi kuhusu masuala ya uzazi.

Unavyoweza kutumia app za kufuatilia hedhi kwa usahihi (na Lucy Protas, Mgunduzi wa Jukwaa la Sports for change).

Inatumia lugha ya Kiswahili

App ya “Hedhi” ni tofauti na apps zingine kwa sababu inalenga zaidi kuwasaidia watumiaji wa lugha ya Kiswahili ambao wanapata changamoto ya kuelewa lugha ya Kiingereza.

“Kwa wanawake ambao hawaelewi Kiingereza wanaweza wasielewe baadhi ya mambo yanayozungumziwa kwenye apps hizo. Kwa app hii inayotumia lugha ya Kiswahili ni nzuri kwao hasa wanaoishi vijijini,” amesema Mwanzilishi wa jukwaa la michezo la Sports for Change, Lucy Protas

Fursa ya kuchati na mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi

Kwa app ya “Hedhi” siyo tu utapata elimu ya afya ya magonjwa mbalimbali yakiwemo saratani ya matiti, bali utaweza kuzungumza na mtaalamu wa masuala ya wanawake kwa kina ili kupata ushauri na nasaha.

Kwa sasa, app hiyo ina madaktari wanne akiwemo daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk Living Colman.

Dk Colman amesema app hiyo itawasaidia akina mama ambao wamekuwa wakiogopa kuonana na madaktari wa masuala ya uzazi. 

“Tunafurahi hatua hii ya kutoa ushauri kwa akina mama na kuwahakikishia kuwa taarifa inayotolewa ni siri kati ya mtoaji na mpokeaji. Tutakuwa tunajadili mada mbalimbali kuhusu mambo muhimu  na hasa yanayohusu mzunguko wa hedhi na mfumo wa uzazi,” anasema Dk Colman. 


Soma zaidi


Manunuzi ya bidhaa za hedhi

Watumiaji wa app ya Hedhi watapata fursa ya kununua bidhaa za hedhi ikiwemo taulo za kike kwa kutumia malipo ya mtandaoni ikiwemo huduma ya kifedha ya M-Pesa ya kampuni ya Vodacom Tanzania. 

Afisa Mawasiliano wa AnuFlo, Myoma Kapya amesema huduma hii bado inafanyiwa maboresho na huenda ikakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo, wamiliki wa app hiyo wanaangalia uwezekano wa kuboresha huduma ili kuwafikia wanawake wa vijijini ambao wengi wao hawana simu zenye intaneti.