Tanzania yaanza kutumia helikopta kuzima moto Mlima Kilimanjaro
Pia inakusudia kuongeza ndege nyingine ili kusaidia zoezi la kuzima moto huo.
- Inakusudia kuongeza ndege nyingine ili kusaidia zoezi la kuzima moto huo.
- Moto huo umeteketeza mabanda 12 ya watalii na mitambo miwili ya umemejua.
- Serikali yawatoa hofu watalii, yasema hali ni shwari.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza kutumia helikopta ili kuongeza kasi na ufanisi wa kudhibiti moto uliozuka Mlima Kilimanjaro mwishoni mwa wiki.
Moto huo ulizuka Jumapili Oktoba 11, 2020 katika eneo la Whona ambacho ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema wameamua kutumia helikopta ili kuongeza ufanisi wa kuzima moto huo ambao kwa sehemu kubwa umedhibitiwa.
“Ili kuongeza ufanisi wa zoezi hilo, leo mchana tumeanza kutumia helikopta,” amesema Dk Kigwangalla katika taarifa yake iliyotolewa Oktoba 15, 2020.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya mikakati ya kuongeza ndege kusaidia zoezi hilo.
Waziri huyo amesema kazi ya kudhibiti moto huo ni ngumu na kubwa tofauti ilivyodhaniwa awali kutokana na changamoto ya upepo mkali na kukauka kwa nyasi na vichaka.
Soma zaidi:
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania
- Tanapa yaendelea kuchunguza chanzo cha moto Mlima Kilimanjaro
- Moto wazidi kudhibitiwa Mlima Kilimanjaro
Hata hivyo, amesema Serikali inachukua tahadhari zote ili kuhakikisha usalama wa wageni na vifaa vyao unaimarika bila kuathiri shughuli za utalii ambazo zinaendelea kama kawaida.
Madhara ya moto huo yaliyoripotiwa mpaka sasa ni pamoja na kuteketea kwa mabanda 12 ya wageni, mitambo miwili ya umemejua na vyoo viwili vilivyopo katika kituo cha Horombo.
Jana nilienda kukagua eneo lililoungua kufuatia mlipuko wa moto Mlima Kilimanjaro. Hii ni sehemu ya taarifa ya madhara yaliyojitokeza. #HK
#Kilimanjaro
pic.twitter.com/1iJHqPAXvu— Dr. Kigwangalla, H. (@HKigwangalla) October 15, 2020
Ilichobaini helikopta juu ya mlima
Helikopta hiyo iliyoanza kuruka jana (Oktoba 15, 2020) kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imebaini kuwa kilimita za mraba 95.5 sawa na asilimia 5 ya eneo lote la hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro lenye kilomita za mraba 1,700 limeathirika na moto huo.
Hata hivyo, Tanapa imesema ukaguzi wa anga uliofanyika leo asubuhi umebaini kuwa moto wote umedhibitiwa hasa maeneo ya tambarare ya juu ta mlima.