November 24, 2024

Maswali magumu kwa wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa Tanzania-3

Gharama za harusi hutofautiana kulingana na mila, uwezo wa kiuchumi na mtazamo wa jamii kuhusu ndoa.

  • Gharama za harusi hutofautiana kulingana na mila, uwezo wa kiuchumi na mtazamo wa jamii kuhusu ndoa.
  • Baadhi ya nchi za Ulaya huamini kuwa harusi nzuri ni ile iliyozingatia viwango vya ubora na siyo idadi ya watu.
  • Viongozi wa dini wawataka wanaofunga ndoa kuzingatia miongozo ya kidini kuepuka changamoto za gharama kwenye harusi. 

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiwa na mitazamo tofauti kuhusu  gharama za harusi, baadhi ya watu kutoka nchi mbalimbali duniani hasa Ulaya na Marekani nao wamezungumzia suala hilo kupata mitazamo tofauti inayoweza kuwasaidia vijana wanaotarajia kuingia kwenye ndoa hivi karibuni.

Katika mahojiano ambayo Nukta (www.nukta.co.tz) imefanya na wananchi hao wanaoishi nchi za nje, wanasisitiza kuwa suala la gharama kuwa kubwa au ndogo kwenye harusi hutegemea zaidi na mitazamo ya watu, mila na hali ya kiuchumi ya jamii husika.

Mkazi wa mji wa Texas nchini Marekani, Claire Siza aliyefunga ndoa miaka mitano iliyopita anasema gharama za harusi ni maamuzi ya watu wawili wanaotarajia kufunga pingu za maisha. 

Anasema kwa Marekani ni kazi ya wanandoa kupanga namna ndoa yao itafanyika bila kuingiliwa au kupangiwa na mtu yeyote, jambo ambalo ni tofauti kwa baadhi ya familia za Afrika ambazo wazazi ndiyo hutoa maamuzi ya mwisho kuhusu harusi.

“Ndoa yangu ilikua na watu wachache. Mimi na mume wangu tulikubaliana kusheherekea na familia zetu tu na siku ilipendeza,” anasema Claire.

Claire anasema tafsiri sahihi ya harusi yenye gharama hutegemea mipango au vitu vitakavyofanyika kukamilisha harusi husika.

“Mnaweza kuwa na wageni 10 tu lakini ndoa ikagharimu mamilioni ya pesa. Gharama ya ndoa utaijua katika vitu mtakavyotaka viwepo au vifanyike kwenye siku yenu ya harusi,” anasema mkazi huyo wa Texas aliyeongea na Nukta kwa njia ya mtandao.


Soma zaidi:


Wakati Claire akiamini mipango ya harusi ni ya watu wawili wanaoana, baadhi ya watu wanaamini harusi nzuri ni ile iliyohudhuriwa na watu wengi huku ikitumia gharama ndogo za fedha.

Benard Chavula kutoka Malawi anayetarajia kuoa hivi karibuni anasema ndoa yake atataka ihudhuriwe na watu wengi wakiwemo ndugu na marafiki huku akitumia kiasi kidogo cha pesa katika vitu vinavyohitajika kwenye harusi yake.

Chavula anasema kiutamaduni wanaamini kuwa na watu wengi ndiyo kufanikiwa kwa shughuli yoyote kama usemi wa Kiswahili unavyosema “shughuli ni watu”. 

“Harusi yangu lazima iwe na watu wengi ila vitakavyotumika kuifanikisha ni vya gharama ya kawaida sana,” anasema Chavula.

Kila sherehe ya harusi hutofautiana kulingana na mahitaji na bajeti ya waandaaji. Picha|TopWeddingSites.

Harusi ni ubora siyo gharama 

Katika mtazamo mwingine, gharama inaweza siyo suala muhimu kwa baadhi ya watu lakini ubora wa sherehe ndiyo unapewa kipaumbele hata kama harusi haitatumia fedha nyingi. 

Derrick Hauston kutoka Uingereza mwenye mtoto anayetarajia kuoa Novemba 2020, anasema anatamani ndoa ya kijana wake iwe katika viwango vya juu yaani kila kitu kitakachofanyika kiwe cha kisasa bila kujali gharama yoyote kwani ni siku muhimu katika maisha.

Hauston ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kwa Uingereza, idadi ya watu wanaohudhuria harusi siyo jambo muhimu bali ubora wa ndoa ndiyo unaozingatiwa.

“Huku kwetu hata ukipata watu kumi, “Quality” (ubora wa viwango) ndiyo inazingatiwa.” anasema Hauston. 

Wakati wadau wote wakizungumzia siku ya harusi, Nicole Sessay kutoka Nigeria anasema gharama ya ndoa au harusi huanza wakati wa kutoa mahari hadi kwenye mapumziko baada ya ndoa yaani “honeymoon” nayo yanapaswa kuangalia upya ili kurahisisha mambo. 

Anasema kwa ndoa za Nigeria, harusi hufanyika mbili; ya kimila na ya kawaida, hivyo  gharama huwa mara mbili kwa waandaaji na utamaduni huo bado unaendelea nchini humo. 

Tovuti inayohusu masuala ya biashara ya Business Review imeongelea ndoa mbalimbali za kifahari zilizowahi kufanyika duniani na kuainisha kuwa gharama za harusi hutegemea na idadi ya watu walioalikwa, idadi ya sherehe yaani harusi itafanyika sehemu ngapi tofauti, aina ya wageni waalikwa na matumizi ya fedha katika vitu vitakavyofanikisha harusi.

Padri Collins Chams wa kanisa la Anglikana la Mtakatifu Bartholomeo lililopo Dallas nchini Marekani, anasema pamoja mitazamo tofauti ya watu kuhusu gharama za harusi, muhimu ni kuzingatia miongozo ya imani kwa kila jambo linalofanyika kukamilisha taratibu za harusi. 

“Wakishafungishwa ndoa kanisani haiishii hapo. Vyovyote sherehe itakavyofanyika lazima misingi ya kidini izingatiwe,” anasema Padri Chams.

Kwa upande wako, unafikiri ndoa yenye gharama ni ipi?

Tutumie maoni yako kupitia barua pepe: newsroom@nukta.co.tz au tufuatilie kwenye mitandao ya kijamii Twitter/Facebook: @NuktaTanzania na Instagram: @nuktatz

Ripoti hii imeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Rodgers George na Tulinagwe Malopa