October 7, 2024

Kivuko kipya kuwafuta machozi wananchi Mwanza

Ni kivuko cha Mv Ukara II ambacho kitakuwa kinasafirisha abiria na mizigo katika ya visiwa vya Ukara na Ukerewe.

Kivuko cha Mv Ukara II tayari kimeingia majini katika Ziwa Victoria tayari kuanza safari kati ya kisiwa cha Ukara na Ukerewe. Picha|Mariam John. 


  • Ni waliopoteza ndugu zao katika ajali ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere Ziwa Victoria mwaka 2018.
  • Serikali yajenga kivuko kipya cha Mv Ukara II. 
  • Kivuko hicho kitaacha kazi hivi karibuni ili kurahisisha usafiri kati ya kisiwa cha Ukara na Ukerewe. 

Mwanza. Zaidi ya miaka miwili tangu wakazi wa visiwa viwili vya Ukara na Ukerewe wapoteze wapendwa wao katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Ziwa Victoria, sasa wamepata tumaini jipya la usafiri wa majini. 

Kivuko cha Mv Nyerere kilizama Septemba 20, 2018 wakati kikitoka kisiwa cha Ukerewe kuelekea kisiwa cha Ukara ambapo watu zaidi ya 200 walifariki dunia na wengine kuokolewa wakiwa hai.

Chanzo cha ajali hiyo ambayo Rais John Magufuli alitangaza siku nne za maombolezo kuwakumbuka waliopoteza maisha ilikuwa ni kivuko kubeba abiria wengi kuliko uwezo wake.  

Hata hivyo, neema imewashukia wakazi hao ambao hivi karibuni wataanza kutumia kivuko kipya kilichopewa jina la Mv Ukara II ambacho kilianza kujenga mwaka 2018 kwa gharama ya Sh4.2 bilioni.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle aliyekuwa akizungumza Oktoba 13, 2020 wakati wa zoezi la kukiingiza majini kivuko hicho, amesema kitasaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Ukara na Ukerewe mkoani Mwanza. 

“Kazi iliyobaki ni kupima na kuhakiki uwezo wa kivuko hiki ili kiweze kufanya kazi na kwamba kazi hiyo itafanywa na  wataalam kutoka chuo cha ubaharia kutoka DIT Dar es Salaam (Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam) pamoja na wataalam wa Tasac (Chama cha Uwakala wa Meli),” amesema Maselle.

Amesema kivuko hicho kina urefu wa mita 42 na upana mita 10  ambapo kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300, tani 100 za mizigo na magari 10. 

Kukamilika kwa kivuko cha Mv Ukara kinakamilisha idadi ya vivuko 31 vinavyofanya kazi katika visiwa mbalimbali vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria. 


Soma zaidi: 


Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi anayesimamia sekta ya ujenzi, Elius Mwakalinga amesema kivuko hicho kitasaidia kuboresha huduma za usafiri wa majini kwa wananchi wanaotumia Ziwa Victoria.

“Kivuko hiki kitaanza kazi baada ya siku tatu, wataalam kutoka Tasac watafika hapa kukifanyia ukaguzi kuhakikisha uimara katika kusafirisha binadamu,” amesema Mwakalinga

Amesema mkoa wa Mwanza ni mkoa wa kimkakati katika masuala ya vivuko na feri ambapo mpaka sasa kuna vivuko 31 na kati ya hivyo 16 vipo ndani ya visiwa vilivyopo mkoani Mwaza.


Mv Ukara II kuchochea biashara

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kukamilika kwa kivuko cha Mv Ukara II kutasaidia kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa maziwa makuu.

Amesema uchumi wa mkoa wa Mwanza unakua kwa sababu usafirishaji wa mizigo na abiria unakuwa salama.

Amesema mpaka sasa mkoani humo kuna miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa ikiwemo ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi, ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli mbili pamoja na chelezo uliogharimu zaidi ya Sh153 bilioni.