November 24, 2024

Kicheko kwa wakulima bei ya mahindi ikipanda Tanzania

Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Julai 2020 ilikuwa Sh58,362 ikipanda kutoka Sh56,914 iliyorekodiwa Juni mwaka huu.

  • Imepanda hadi Sh58,362 mwezi Julai kutoka Sh56,914 ya Juni 2020. 
  • Bei ya mazao mengine ya chakula yashuka mwezi Julai.
  • BoT yasema kushuka kwa bei ya mazao ya chakula ni matokeo ya kuongezeka kwa mazao msimu wa mavuno. 

Dar es Salaam. Wakulima na wafanyabiashara huenda wakaendelea kunufaika na kilimo cha mahindi, baada ya bei ya zao hilo kupanda kwa Sh1,448 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, huku ikiiacha maumivu kwa wanunuzi wa chakula nchini Tanzania. 

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Agosti 2020 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Julai 2020 ilikuwa Sh58,362 ikipanda kutoka Sh56,914 iliyorekodiwa Juni mwaka huu.

Bei hiyo ya Julai ni sawa ongezeko la Sh1,448 katika kipindi cha mwezi mmoja. 

Kupanda kwa bei ya mahindi kutawafaidisha zaidi wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo ili kujipatia kipato cha kuendesha familia. 

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele na ulezi.


Soma zaidi: 


BoT katika ripoti hiyo imeeleza kuwa kwa wastani bei za jumla za mazao yote chakula zilishuka mwezi Julai 2020 ikilinganishwa na mwezi uliotangulia wa Juni isipokuwa mahindi.

Bei ya jumla ya mchele imeshuka kutoka Sh152,259 hadi Sh148,991.7; maharage kutoka Sh204,990 hadi Sh192,771.5; na mtama umeshuka kutoka Sh113,321 hadi Sh99,597.9. 

Pia katika kipindi hicho, bei ya jumla ya viazi mviringo imeshuka kutoka Sh81,809 hadi Sh78,222.3 huku uwele ukishuka hadi Sh133,188.5 kutoka Sh134,984.0 Juni mwaka huu. 

“Mabadiliko hayo ni matokeo ya kuanza kwa msimu wa mavuno na soko la mazao yanayokomaa kwa muda mrefu,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Akiba ya chakula yaongezeka

Wakati bei za mazao makuu ya chakula zikipanda na kushuka, akiba ya chakula katika ghala la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. 

Ripoti hiyo imeeleza kuwa akiba ya chakula ya NFRA imeongezeka hadi tani 90,255 mwezi Julai 2020 kutoka tani 52,724.7 mwezi Juni mwaka huu. 

Kiwango hicho cha chakula kwa mwezi Julai ndiyo ni cha juu zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Akiba hiyo ya chakula inajumuisha mahindi, mtama na mpunga ambapo BoT inaeleza kuwa ongezeko la akiba ya chakula limetokana na ununuzi uliofanywa na NFRA katika msimu wa mavuno. 

Mwezi Julai 2020, NFRA ilinunua tani 32,676.7 za mahindi, mpunga (tani 4,088.4) na mtama (tani 829.5) ambapo iliuza tani 64.3 za mahindi kwa Jeshi la Magereza. 

Mwenendo wa uhifadhi wa chakula katika ghala hilo ambalo huifadhi chakula kwa ajili ya dharura kama njaa umekuwa wa kupanda na kushuka katika miaka mitano iliyopita.