Haya ndiyo masoko ya maua Tanzania
Ni pamoja na wadau wa sherehe na mtu mmoja mmoja ambao huyapata maua hayo kwa gharama inayoanzia Sh1000.
- Sherehe mbalimbali ambazo zinahitaji mapambo na muonekano tofauti zikiwemo harusi.
- Maua pia yanatumika kwenye misiba kuwafariji na kuwapunguzia huzuni wafiwa.
- Hata hivyo, muamko wa Watanzania kutumia maua bado siyo mkubwa.
Dar es Salaam. Wakati ukiwaza ni biashara gani ufanye, basi kuuza maua ya asili inaweza kuwa biashara sahihi kwako kutokana na kuwepo kwa soko la ndani la Tanzania lililosheheni wateja wenye mahitaji mbalimbali.
Maduka ya maua yaliyopo Mbuyuni, Osterbay jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa maeneo ambayo yanasifika kwa uuzaji wa bidhaa hizo nchini.
Eneo hilo ambalo limekuwa kivutio kwa wanunuzi wa maua, ni sehemu muhimu kwa Watanzania waliowekeza katika biashara hiyo kujipatia kipato.
Maua yanayouzwa Osterbay ni pamoja na yale yanayoagizwa kutoka nchini Kenya na jijini Arusha ambako kuna hali ya hewa nzuri inayoruhusu kilimo hicho.
Uzuri wa maua hayo yenye muonekano na harufu tofauti, ndiyo yamekuwa yakiwavutia watu wanaotumia barabara ya Bagamoyo inayopita katikati ya jiji kufika hapo ili kujipatia maua kukidhi mahitaji yao.
Navutiwa zaidi kuingia katika duka moja la Haika Florist lilipo Mbuyuni ambalo nje ya duka hilo kuna watu wanaendelea na shughuli zao ikiwemo kutengeneza vifurushi vya maua, kupamba fremu za picha za marehemu.
Maua hayo yako aina mbalimbali ikiwemo mawaridi (roses) na maua ya yungiyungi (Tiger lilies) na majani ya aina mbali mbali ni kati ya maua ambayo watu hufika hapo kujichagulia kwa ajili ya madhumuni wanayoyafahamu wao.
Hapo nakutana na mmiliki wa duka hilo, Haika Kimaro ambaye ananielewesha kwa undani mwenendo na soko la maua, ambalo linaweza kuwa fursa hasa kwa vijana kuwekeza katika biashara hiyo.
Maua hayo yanayopatikana Osterbay jijini Dar es Salaam hutumika kwa shughuli mbalimbali sherehe na misiba. Picha| Rodgers George.
Sherehe mbalimbali
Kama wewe ni mhudhuriaji wa sherehe za harusi, “send off”, “kitchen party”, basi utakuwa siyo mgeni wa maua yenye muonekano na harufu tofauti.
Wengi wanaamini sherehe haiwezi kunoga kama haina vionjo vya mapambo ya maua ya asili, basi hapo wajasiriamali hujipatia fedha zao.
“Tofauti na zamani, maua asilia yameshika soko. Zamani watu walipenda kutumia maua bandia kwenye sherehe zao lakini siku hizi watu wanasafirisha maua hadi Bukoba mkoani Kagera) kwa ajili ya harusi,” amesema Kimaro anayeuza maua hata kwa mtu mwenye bajeti ya Sh1,000.
Anasema wateja wake wengi ni waandaji na wapambaji wa sherehe, jambo linalofanya biashara kuwa nzuri siku ya Jumatano, Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi.
Misibani na kumbukizi za misiba
Wakati nikitoka kwenye duka la Kimaro, nakutana na kijana Ramadhan Bunga ambaye kazi yake ni kuwatengenezea wafiwa mashada na fremu za maua kabla hayajapelekwa kwenye shughuli husika.
Bunga ambaye nimemkuta akipamba picha ya mtoto ambaye amefariki, anasema kazi hiyo ndiyo inamuweka mjini kwa sababu maua huitajika msibani kuwafariji wafiwa na kuonyesha upendo kwa mtu aliyefariki.
“Maua msibani yana kazi yake. Kwa namna ya ajabu, mimea hiyo huweza kupunguza huzuni. Rangi nyeupe ni ishara ya amani na ndiyo maana misibani tunaweka maua meupe. Ni kitu kisichoweza kuelezeka lakini mtu ukiona rangi nyeupe, unajihisi amani,” amesema Bunga.
Maua kwa baadhi watu huonyesha hisia za upendo kwa mtoaji na mpokeaji. Picha| freepik.com
Wapendanao nao hawako nyuma
Licha ya kuwa mahusiano hutegemea upendo unaotoka moyoni, lakini maua yana sehemu ya kunogesha upendo na hisia kwa wapendanao.
Bunga ambaye hufanyia shughuli zake karibu na kanisa la St Peters Oyserbay, amesema maua yana maana kubwa kwa wapendanao.
“Wenzetu wanafahamu maua. Maua yanaongea. Ni vitu vidogo vidogo kwenye mapenzi ya kweli ndiyo hujenga mahusianp. Ni pamoja na kumpa mpenzi wako maua. Ni kitendo cha kufahamu kuwa unafikiria,” amesema Bunga ambaye amesema wateja wake wengi ni Wazungu, Waarabu na Wahindi.
Hata hivyo, Bunga amesema Watanzania wengi hufurika zaidi eneo la Mbuyuni kujipatia maua siku kuu ya wapendanao (Valentine Day) inayofanyika Februari 14 kila mwaka, jambo linalowafanya wauze maradufu.
“Maua siku hiyo huwa hayatoshi. wachache wananunua kwa ajili ya siku za kumbukizi za kuzaliwa,” amesema Bunga ambaye anauza kifurushi kimoja chenye maua mchanganyiko kwa Sh10,000.
Soma Zaidi:
- Fursa uzalishaji wa maua Tanzania
- Sababu za wabunifu wa nguo kutumia malighafi za nje
- Utalii wa farasi unavyoweza kubadilisha mtazamo wako wa matembezi
Masoko mengine
Mbali na masoko hayo ambayo ni makuu kwa wauza maua, yapo masoko mengine ambayo yenyewe ni ya msimu.
Mahitaji mengine ya maua ni pamoja na kuwapelekea wagonjwa hospitalini, pongezi na mahafali ya kuhitimu ngazi fulani ya elimu ikiwemo elimu ya juu.
“Soko la maua ni kubwa sana. Wapo hadi wanaonunua maua kwa ajili ya kuweka ndani kwao na wengine maofisini,” anasema mkazi wa jijini Arusha, William Peter ambaye yeye hunua maua kwa ajili ya kuombea msamaha kwa rafiki zake.
“Kila ua lina maana yeka na hata rangi yake pia ina maana,” amesema Peter.
Kufahamu maana ya rangi za maua, usikose muendelezo wa makala haya kesho ambapo tutaangazia pia mitazamo ya watu kuhusu maua kwenye mahusiano.