Wakandarasi watakiwa kuongeza kasi ujenzi meli ya Mv Mwanza
Serikali yasema zoezi la uundwaji wa meli hiyo linatakiwa kukamilika kwa wakati kama mkataba ulivyosainiwa.
- Serikali yasema zoezi la uundwaji wa meli hiyo linatakiwa kukamilika kwa wakati kama mkataba ulivyosainiwa.
- Uundwaji wake umefikia asilimia 60 tangu ulipoanza Machi 2018.
- Kukamilika kwa meli kutasaidia kupunguza changamoto ya usafiri wa majini kwa wakazi wanaotumia Ziwa Victoria.
Mwanza. Serikali imewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza kuhakikisha zoezi la uundwaji wa meli hiyo linakamilika kwa wakati kama mkataba ulivyosainiwa.
Ujenzi wa meli hiyo mpya ulianza mwezi Machi 2018 kwa gharama ya Sh90 bilioni, ujenzi ambao ulihusisha pia utengenezwaji wa chelezo ambayo tayari imekamilika na kukabidhiwa serikalini mwanzoni mwa mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amesema licha ya kazi nzuri inayofanywa na wakandarasi wanaojenga meli hiyo, wanatakiwa kuongeza kasi ili zoezi hilo likamilike kwa wakati.
Kukamilika kwa meli kutasaidia kupunguza changamoto ya usafiri wa majini kwa wakazi wanaotumia Ziwa Victoria.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za meli Tanzania (MSCL), Eric Hamissi amesema meli hiyo ni tofauti na zingine kwa sababu yenyewe inaundwa hapa nchini.
“Tunajua tulikuwa na meli kubwa ya Mv Victoria ambayo imekarabatiwa na sasa inaitwa Mv New Victoria hapa kazi tu ambayo iliundwa miaka 60 iliyopita na kwamba haikuundiwa hapa nchini.
“Sasa meli hii mpya ya Mv Mwanza leo inaundwa hapa nchini na itafungua milango kwa nchi zingine kufika na kuunda meli zao,” amesema Hamissi aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 16, 2020) wakati wa zoezi la kuweka mgongo juu ya chelezo ikiwa ni hatua ya kwanza ya uundwaji wa meli hiyo.
Zinazohusiana:
- Zanzibar, kitovu utengenezaji wa meli Afrika Mashariki
- Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai
- Rais Magufuli atangaza siku nne za maombelezo ya waliofariki katika ajali ya Mv Nyerere
Hamissi mesema hatua hiyo ni kwanza katika uunganishaji wa msingi wa meli ili ianze kuundwa.
Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo kwa sasa imekamilika kwa asilimia 68 kwa maana ya kukata vyuma na kuunganisha vipande vyote ambavyo zitapandishwa juu ya chelezo.
Eric amesema ili meli mpya ikamilike hupita hatua nne mhimu ambazo ni ujenzi wa msingi wa meli, kushusha meli majini, uzinduzi wa meli pamoja na kukagua meli kama vyombo vyake viko salama.
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kimataifa ya Kikanda ya CCTTFA, imefadhiri Sh209.4 milioni kama gharama za kusomesha watumishi wa MSCL katika kozi mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanidi.
“Makubaliano yaliyosainiwa leo yatadumu kwa kipindi cha miaka mitatu na yamehusisha ufadhili wa mafunzo kwa watumishi wa kada zote kuanzia mabaharia hadi menejimenti ya MSCL,” amesema Hamissi.
Mafunzo hayo yatatolewa katika vyuo vitatu: Chuo cha Bahari cha Dar es Saalam(DMI), Chuo cha Usafiri cha Taifa (NIT) na Chuo Cha Uzalishaji Cha Taifa ( NIP).