October 7, 2024

Ndoa sio mafanikio pekee kwa mtoto wa kike

Umuhimu uliowekwa katika ndoa unafanya wanawake wengi wakae katika ndoa ambazo haziwapi furaha.

  • Huu umuhimu uliowekwa katika ndoa unafanya wanawake wengi wakae katika ndoa ambazo haziwapi furaha.
  • Heshima ya mwanamke imefungwa katika kuwa na pete kidoleni au kutokuwa na pete.
  • Ndoa ni vitu vingi, lakini si uwanja wa mapigano. Ndoa inapokuwa ndoano si ndoa tena.

Nilipokuwa mdogo, fikra zangu kuhusu ndoa hazifanani na hizi za sasa. Mimi kama watoto wengine wa kike nilikuwa na ndoto ya kuja kuolewa.

Mara nyingi nilikuwa niki ‘imagine’ (fikiria) ndoa yangu itakavyokuwa. Gauni jeupe, maua, mume mzuri anayenipenda na tutakuwa na kila kitu ambacho watu wengi tunataka kuwa nacho. Nyumba nzuri, magari mazuri n.k.

Nilipokuwa katika masomo ya kidato cha tano na sita, nikawa nafikiri nitaolewa nikifika chuo mwaka wa pili kwa sababu nitakuwa nimekua, nitapata mwanaume atakayenipenda, atakuwa mwaminifu na atataka tuoane, tuishi wote.

‘Spoilers alert’ (Jambo la ajabu), bado sijaolewa mpaka sasa.

Mawazo ya kuolewa yanapandikizwa katika akili za watoto wa kike tangu tukiwa wadogo sana. Kujifunza kupika, (kama hujui kupika basi huwezi kupata mume) kuwa msafi, kuvaa vizuri na vingine vingi vinahusishwa na wewe kupata mume. 

Unapokuwa umefanikiwa kupata pesa, kufanya kazi nzuri au kuwa na biashara zako, unaambiwa usijioneshe sana utakosa mume. Mafanikio yako na pesa zako zitawatisha wanaume na hawatakuona kama ‘wife material’ (mke mwema).

Ndoa ni vitu vingi, lakini si uwanja wa mapigano. Ndoa inapokuwa ndoano si ndoa tena. Picha| Stenzel Clinical Services. 

Mtazamo wa jamii kuhusu wanawake

Katika jamii zetu, hasa za Kitanzania (ndio jamii ninayoifamu vizuri) mafanikio ya mwanamke yanaonekana pale tu anapokuwa ameolewa. Anapokuwa na mafanikio katika nyanja nyingine za maisha yake, bado swali kubwa huwa “umeolewa?” “unaolewa lini”?

Heshima ya mwanamke imefungwa katika kuwa na pete kidoleni au kutokuwa na pete. Unapoonekana una pete, utapewa heshima.  Unapokosa pete, hata ile heshima unayostaili huipati.

Vitu kama hivi vinachangia sana kwa wanawake kukimbilia kuolewa hasa anapofikisha umri wa miaka 30. Jamii yetu imefanya wanawake kujiona wamefikia ‘expire date’ wanapofika umri huu. 

Utasikia kauli kama “yeyote atayekuja sasa naolewa naye” bila hata kuangalia kama ni mtu mnayependana na kuheshimiana, anayefaa kuishi naye na kuanzisha naye familia. 

Huu umuhimu uliowekwa katika NDOA unafanya wanawake wengi wakae katika ndoa ambazo haziwapi furaha. 

Wanawake wanakaa kimya hata pale wanapoambulia ‘vipigo vya mwizi’ na manyanyaso kutoka kwa waume zao ambao walipaswa kuwalinda, kuwapenda na kuwaheshimu kwa sababu tu hawawezi kusema kama wanapigwa. 


Soma zaidi: 


Na hata wakipata ujasiri wa kusema kwa ndugu zao na marafiki wataambiwa VUMILIA. Ndoa ni uvumilivu. Usione ndoa za watu zimedumu, wao pia wanavumilia na kupitia mengi. 

Mwanamke atajitahidi kusema: lakini ninapigwa sana na mume wangu. Ataambiwa: haiwezekani UKAPIGWA bila kosa, lazima umefanya kitu ndiyo maana UMEPIGWA. 

Atakapopata ujasiri wa kuondoka katika ndoa hiyo ambayo imegeuka kuwa ndoano kuna changamoto zingine zinamsubiri. Maneno lukuki huibuka. “Ndoa imemshinda, amevunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe…tulijua tu hawezi kudumu,” watasema.

Kuna kesi ngapi tumezisikia zikiripotiwa kwamba kuna mwanamke ameuwawa na mume wake? Kesi ngapi ambazo hazijaripotiwa? Wanawake wangapi wanaendelea kukaa kimya kwa kuogopa watakachoambiwa na jamii baada ya kusema?

Mpaka lini tutafumbia macho visa hivi vya wanawake kupigwa mpaka wengine kufikia umauti kwa sababu tu jamii inaendelea kuaminisha watoto wa kike kwamba hawajapata mafanikio mpaka watakapopata mume na ndoa?

Ndoa ni kitu kizuri ikiwa wote wawili mtakuwa na furaha na mtaheshimiana kama binadamu. Ndoa ni makubaliano ya watu wawili, ambao wameamua kupendana na kuishi pamoja. Ndoa si sehemu ya mwanamke au mwanaume kunyanyasika. 

Unampiga vipi mtu unayesema unampenda na ukaamua kuishi naye ndani ya ukuta mmoja na kuwa “mwili mmoja”?

Ndoa ni vitu vingi, lakini si uwanja wa mapigano. Ndoa inapokuwa ndoano si ndoa tena.

Lazima pia tufahamu kuwa ndoa ni kitu kizuri lakini si mafanikio pekee kwa mtoto wa kike.