Yatakayosaidia kupunguza vifo vya wanyamapori Tanzania
Ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya kamera za kudhibiti mwendokasi wa magari kuwaepusha wanyamapori na ajali za barabarani.
- Ni vile vinavyosababishwa na ajali zinazotokea kwenye barabara zilizopita kwenye hifadhi za Taifa.
- Wadau washauri matumizi ya kamera za kudhibiti mwendokasi na ushirikiano wa kisekta.
Dar es Salaam. Wadau wa mazingira wamependekeza njia mbalimbali zitakazosaidia kupunguza vifo vya wanyamapori vinavyosababishwa na ajali za barabarani zinazopita kwenye hifadhi za Taifa ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa za kudhibiti mwendo kasi wa vyombo vya moto.
Baadhi ya hifadhi za Taifa ikiwemo ya Mikumi imepitiwa na barabara kuu ya kutoka jijini Dar es Salaam hadi jijini Mbeya, jambo ambalo limekuwa likileta changomoto kwa wanyamapori wanaokatiza kwenye barabara hizo, licha ya Serikali kuweka mikakati mbalimbali ya kuwalinda.
Mtaalam wa wanyamapori kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) linalosimamia mradi wa uhifadhi wa PROTECT, Exper Pius amesema matumizi ya teknolojia ikiwemo kamera maalum za kufuatilia amwendo kasi wa madereva katika maeneo ya hifadhi yatasaidia kupunguza vifo vya wanyama hao.
“Tutumie teknolojia kwa maana kwamba katika barabara zinazopita kwenye hifadhi tuweke kamera za kufuatilia mwendo wa magari ili dereva akiendesha kwa mwendo usiofaa (kasi) achukuliwe hatua ikiwemo kupigwa faini,” amesema Pius leo (Septemba 12, 2020) katika mafunzo ya mtandaoni ya uhifadhi wanyamapori yaliyoandaliwa na USAID-Protect na Chama Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).
Pius amesema njia nyingine ya kunusuru maisha ya wanyamapori ni kuwatengenezea njia zao (bypass) ambazo ni tofauti na barabara za magari zinazokatiza kwenye hifadhi za Taifa.
Amesema hiyo itasaidia kupunguza muingiliano wa wanyamapori na vyombo vya moto, jambo linaweza kutekelezeka ikiwa mipango mizuri itawekwa wakati wa kujenga barabara kwenye hifadhi ili kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kuishi ili kuifaidisha nchi katika shughuli za utalii.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Wakati Pius akihimiza teknolojia kuwalinda wanyamapori, Mwenyekiti wa JET, Dk Hellen Otaru amesema ushirikiano wa wadau kutoka sekta mbalimbali ni muhimu kusaidia katika kupunguza vifo vya wanyamapori vinavyotokana na ajali.
“Kuna umuhimu wa wadau wengi kuongeza nguvu kukabiliana na tatizo hilo kuwe na watu wengi zaidi ambao watasaidia katika uhifadhi wanyamapori,” amesema Dk Otaru.
Sambamba na hilo, mtaalam huyo wa mazingira amesema mipango bora ya matumizi ya ardhi hasa inayohusisha binadamu na wanyamapori izingatiwe ili kuwe na mipaka itakayosaidia kupunguza matukio ya ajali.
Mipango hiyo ni ile inayozingatia mapitio ya wanyama (shoroba) na maeneo ambayo wananchi hawatakiwi kufika kwenye hifadhi za wanyama.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mashirika ya umma kwa mwaka 2018/2019 inaonyesha kuwa jumla ya wanyamapori 2,266 waliuawa katika mwaka ulioishia Juni 30, 2019 kutokana na ajali za barabarani katka hifadhi mbalimbali za Taifa nchini.
Kati ya wanyamapori hao waliouawa, 124 walikuwa wa hifadhi ya Taifa ya Mikumi (Minapa). CAG Charles Kichere anaeleza katika ripoti hiyo kuwa kazi nzuri ya ufatiliaji wa karibu wa mauaji ya wanyamapori inafanyika na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro kwenye barabara kuu.
Lakini amesema kuna changamoto mbalimbali zinazosababishwa na kuwa na teknolojia duni ikiwemo kukosa kamera za barabarani jambo linalosababisha kushindwa kutambua wahusika wanaosababisha ajali hizo.
“Ninapendekeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro zitunge sheria ndogo na kuzisimamia ipasavyo. Aidha, zibuni na kusimamia njia mbalimbali za usalama kama vile kuweka kamera za barabarani ili kudhibiti ajali za barabarani na hivyo kulinda wanyamapori,” amependekeza CAG Kichere.