Kulikoni walimu kupungua shule za msingi za Serikali Tanzania?
Mazingira yasiyoridhisha ya kazi ni moja ya sababu zinazochangia hali hiyo huku Serikali ikisema itaendelea kuongeza idadi ya walimu ili kukidhi mahitaji.
- Tangu mwaka 2017 idadi ya walimu katika shule za msingi za umma imekuwa ikipungua kila mwaka.
- Mazingira yasiyoridhisha ya kazi ni moja ya sababu zinazochangia hali hiyo.
- Idadi ya wanafunzi katika shule za msingi inendelea kuongezeka kila mwaka.
- Serikali yasema itaendelea kuongeza walimu kukidhi mahitaji.
Dar es Salaam. Wakati kasi ya uandikishaji wanafunzi katika shule za msingi nchini Tanzania Bara ikiongezeka kila mwaka, imedhihirika kuwa idadi ya walimu katika shule za Serikali imekuwa ikipungua kwa miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2017, jambo linalopunguza jitihada za kutoa elimu bora nchini.
Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania ya mwaka 2019 (Tanzania in Figure 2019) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Juni mwaka huu, inaonyesha kuwa udahili wa wanafunzi katika shule za msingi za Serikali na binafsi Tanzania Bara umekuwa ukiongezeka kila mwaka tangu mwaka 2016.
Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila mwaka, inaeleza kuwa mwaka 2019, wanafunzi milioni 10.6 waliandikishwa katika shule za msingi ikilinganishwa na wanafunzi milioni 8.3 waliondikishwa mwaka 2015.
Kati ya wanafunzi hao walioandikishwa mwaka 2019, asilimia 96 wanatoka katika shule za umma ambazo zimeshuhuduia ongezeko hilo likichangiwa na sera ya elimu bila malipo iliyoanza kutekelezwa mwaka 2016 kwa shule za msingi, kidato cha kwanza hadi cha nne.
Sera hiyo ilitoa hamasa kwa wazazi na walezi hasa wenye kipato cha chini kuwapeleka watoto wao shule ili wakapate elimu na kutimiza ndoto zao.
Licha ya ripoti hiyo ya NBS kubainisha kuwa uandikishaji unaongezeka kila mwaka lakini idadi ya walimu katika shule za msingi zinazomilikiwa na Serikali imekuwa ikishuka mfululizo kwa miaka mitatu iliyopita.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka 2018 shule za Serikali zilikuwa na walimu 191,771 lakini mwaka uliofuata walipungua hadi 188,336 kabla ya kushuka zaidi hadi 182,002 mwaka jana.
Kwa takwimu za wanafunzi na walimu wa shule za Serikali waliokuwepo mwaka 2019 ni sawa na kusema kwa wastani mwalimu mmoja alikuwa akifundisha takriban wanafunzi 56 katika darasa moja (1:56), ikiwa juu ya wastani unaopendekezwa na Serikali wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi wasiozidi 45 (1:45).
Wakati idadi walimu katika shule za msingi za Serikali ikipungua, katika shule binafsi idadi imekuwa ikongezeka sambamba na uandikishaji wanafunzi kila mwaka tangu 2016. Mwenendo wa uandikishaji wanafunzi katika shule binafsi unafanana karibu na ule wa shule za umma.
Mathalan, hadi kufikia mwaka jana shule binafsi zilikuwa na walimu 26,768 ambapo waliongezeka kutoka 13,178 waliokuwepo mwaka 2015 sawa ongezeko la zaidi ya mara moja katika kipindi cha miaka minne.
Kwa takwimu za mwaka jana katika shule hizo ambazo ziliandikisha wanafunzi 431,193, mwalimu mmoja anafundisha wastani wa takriban wanafunzi 33 katika darasa moja (1:33).
Uwiano huo au kiwango hicho ni bora zaidi ya kile kinachoshauriwa cha mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45, jambo linalotoa fursa kwa walimu kuwafikia wanafunzi vizuri darasani ili kupata maarifa na ujuzi.
Sababu za kupungua kwa walimu shule za Serikali
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaeleza kuwa sababu nyingine ya kupungua kwa idadi ya walimu ni kupanuka kwa sekta nyingine zenye maslahi mazuri.
“Baadhi ya walimu wamekuwa wakiacha kazi ya ualimu na kujiunga na sekta ambazo zinavutia zaidi kimaslahi na mazingira,” inasomeka sehemu ya sera hiyo.
Zinazohusiana:
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari
- Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba
- Hisabati, Kiingereza bado pasua kichwa mitihani darasa la Saba Tanzania
Mwaka 2017 wakati idadi ya walimu ilipoanza kupungua, ndiyo kipindi ambacho Serikali iliendesha zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma nchi zima ambapo walimu 3,655 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na kupoteza sifa za kuendelea kuwa watumishi wa umma.
Mchambuzi wa masuala ya elimu Richard Mabala anasema katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Serikali imewekeza zaidi rasimali zake katika uboreshaji wa miundombinu ikiwemo madarasa na vifaa vya kusomea ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi.
Anasema huenda hali hiyo imechangia kutokuongeza walimu katika kiwango cha kukidhi mahitaji ya wanafunzi.
“Walimu wengi wamehitimu lakini hawajaajiliwa nadhani sababu mojawapo ni hiyo. Ni vipaumbele vya Serikali fedha kutumika kwa vitu vingine ikiwemo kuboresha miundombinu ya shule,” anasema Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hakielimu.
Athari kwa wanafunzi
Humfrey Kimbisa, mzazi wa mwanafunzi anayesoma katika Shule ya Msingi Simike mkoani Mbeya ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) uhaba wa walimu unawafanya wanafunzi kukosa maarifa sahihi kuwawezesha kujibu mitihani yao.
“Naamini Serikali italifanyia kazi hili kuongeza idadi ya walimu kila mwaka ili kuhakikisha wanafunzi wanapewa kipaumbele,” anasema Kimbisa.
Anasema hali hiyo ina athari kubwa kwa maendeleo ya wanafunzi kwa sababu wakiwa wengi wanakosa maarifa na ujuzi kutoka kwa walimu ambao wana mchango mkubwa kufanikisha ndoto zao.
Mbali na Serikali kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya shule, wadau wanashauri pia rasilimali watu isisahaulike kwa kiwango kikubwa.
“Inabidi kupanga mipango ya kuhakikisha kwamba walimu na miundombinu inatosheleza uongezekaji wa watoto. Miundombinu italeta matokeo lakini ni muhimu kutumia miundombu watu ili kuleta matokeo mazuri zaidi shuleni,” anasema Mabala.
Mafanikio ya elimu kwa wanafunzi yanategemea zaidi waalimu kuwepo na kufundisha darasani. Picha| Zahara Tunda.
Mikakati ya Serikali kuongeza walimu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Selemani Jafo na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mwita Waitara hawakuweza kupatikana kwa wakati kuzungumzia mwenendo huo wa kushuka kwa walimu katika shule za msingi za umma.
Hata hivyo, Jafo akizungumza Agosti 4, 2020 katika wiki ya elimu ya wizara yake jijini Dodoma alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imeajiri walimu zaidi ya 18,100 ambapo wamepelekwa katika shule za msingi na sekondari.
“Lengo kubwa walimu hawa wakaongeze nguvukazi kwa ajili ya vijana waweze kupata elimu,” alisema Jafo.
Jafo alisema Serikali itaendelea kuboresha maslahi na idadi ya walimu ili kukidhi ongezeko la wanafunzi kuwawezesha kupata elimu bora.
“Hata hivyo, ninafahamu bado kuna changamoto zingine na ndiyo maana Mheshimiwa Rais (John Magufuli) alitoa maelekezo ajira za walimu zingine zitolewe,” alisema waziri huyo huku akisisitiza kuwa taratibu za kuajiri walimu 12,000 wa msingi na sekondari zinaendelea.
Hata wakati walimu walioajiriwa katika shule za umma wakipungua, vyuo vya ualimu nchini navyo vinapungua.
Ripoti hiyo ya takwimu muhimu ya NBS inaeleza kuwa mwaka 2019 kulikuwa na vyuo vya ualimu 88 vilivyopungua kutoka 137 vilivyokuwepo mwaka 2018, kutokana na kufungwa kwa vyuo 49 vilivyokuwa vinamilikiwa na watu binafsi.