November 24, 2024

Wakulima kulipwa Sh12 bilioni za kahawa Kagera

Ni fedha walizouza kahawa kwa vyama vya ushirika mkoani humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (katikati) akiongea na waandishi wa habari leo jijini Mwanza kutangaza uamuzi wa kuanza kuwalipa wakulima wa kahawa wa mkoa wa Kagera fedha zao Sh12 bilioni kupitia Vyama Vikuu vya KDCU na KCU.Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe. Picha|Wizara ya Kilimo.


  • Ni fedha walizouza kahawa kwa vyama vya ushirika mkoani humo.
  • Deni hilo linatokana na Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KDCU) kuendelea kukusanya kahawa ya wakulima. 
  • Watanzania watakiwa kunywa kahawa kwa wingi kukuza soko la ndani. 

Dar es Salaam. Huenda wiki hii ikiwa ni kicheko kwa wakulima wa kahawa mkoani Kagera, baada ya Serikali kuahidi kuwalipa madeni yao ya Sh12 bilioni yanayotokana na uuzaji wa zao hilo kwa vyama vya ushirika mkoani humo. 

Serikali imesema wakulima waliokusanya kahawa yao kwenye vyama vya ushirika mkoani Kagera wataanza kulipwa madeni yao mapema wiki hii.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema tangu msimu wa ununuzi wa kahawa ulipofunguliwa mwezi Juni mwaka huu, Sh32 bilioni tayari zimelipwa kwa wakulima wa Kagera kutokana na kukusanya tani 62,336 za kahawa ghafi na tani 31,168 za kahawa safi kwenye vyama vikuu vya ushirika na vile vya msingi.

Kusaya aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 1, 2020) jijini Mwanza amesema pamoja na kulipa Sh32 bilioni za wakulima bado Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KDCU) kinadaiwa Sh12 bilioni kutokana na kukusanya kahawa ya wakulima.

“Kikao chetu cha leo tumekubaliana KDCU waanze kulipa wakulima Sh7 bilioni zilizopo tayari kuanzia kesho na zingine Sh5 bilioni zitalipwa mapema wiki ijayo,” amesema Kusaya katika kikao cha viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, mikoa ya Mwanza na Kagera na vyama vikuu vya Ushirika  KDCU na KCU.

Katibu Mkuu huyo amesema deni hilo linatokana na KDCU kuendelea kukusanya kahawa ya wakulima kufuatia uwepo wa mavuno mazuri.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, vyama hivyo vinakusanya kahawa yenye thamani ya Sh1.7 bilioni kila siku na tayari wamenunua kilo milioni 37.3 kati ya lengo la kilo milioni 45 za kahawa msimu huu.


Soma zaidi:


Katika taarifa iliyotolewa na wizara yake, Kusaya amesema kuwa madeni ya wakulima wa kahawa yatalipwa kadiri wanunuzi wanavyotoa fedha kwa vyama vya ushirika

“Sh2 bilioni za wakulima waliouza kahawa KCU tumekubaliana zitaanza kulipwa wiki hii Kagera na kuwa zingine Sh3 bilioni zitatolewa na mnunuzi aliyeuziwa kahawa na KCU katika muda mfupi ujao” amesisitiza Kusaya.

Hata hivyo, malipo hayo yamechelewa kwa sababu vyama vikuu vya ushirika kuchelewa kuuza kahawa kwa wanunuzi. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Kahawa Tanzania, makusanyo ya kahawa msimu wa 2020/21 yamefikia ya tani 79,245 (asilimia 73) kati ya lengo la tani 108,000 na tani 44,695 (asilimia 63) za kahawa safi kati ya lengo la tani 70,000. 

Kahawa hiyo imekusanywa toka kwenye mikoa yote 17 inayolima zao la kahawa nchini ikiwemo Kilimanjaro na Mbeya. 

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora amesema wakulima wa kahawa msimu huu wamepata bei nzuri karibu asilimia 75 ya bei ya soko la dunia na kuwa KDCU na KCU kwa mkoa wa Kagera wamefanya kazi nzuri kuwezesha wakulima kulipwa bei nzuri.

Prof Kamuzora ametoa wito kwa Watanzania kuwa na tabia ya kunywa kahawa ili kusaidia upatikanaji wa soko la kahawa ndani ya nchi tofauti na ilivyo sasa kahawa asilimia 93 inayozalishwa nchini inauzwa nje ya nchi.