Tanzania yaweka tozo mpya kwa watalii 2020-21
Wageni wanaotoka nje ya Afrika Mashariki kulipa zaidi ya wazawa.
- Ni tozo za viingilio kwenye hifadhi za Taifa.
- Wageni wanaotoka nje ya Afrika Mashariki kulipa zaidi ya wazawa.
- Zitatumika katika mwaka wa fedha wa 2020/21.
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikifungua milango kwa watalii baada ya kutokomezwa kwa janga la Corona, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imetoa orodha ya tozo za viingilio katika hifadhi inazosimamia ambazo zitadumu kwa mwaka 2020/21.
Kwa sasa Tanzania ina hifadhi za Taifa 22 baada ya kuanzishwa kwa hifadhi sita mpya za Nyerere, Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa, Kigosi, Ugalla River na Rumanyika-Karagwe mwaka jana.
Wakati ukipanga bajeti yako utakayotumia katika hifadhi hizo, una kila sababu ya kufahamu tozo hizo kwa undani ili ufanikishe safari ya mapumziko na kujifunza vitu vipya.
Tozo hizo zinazotozwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi. ni za kipindi cha mwaka mmoja na tayari zimeanza kutumika tangu Agosti 1, 2020 na zitadumu hadi Juni 30, 2021.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) wa tozo hizo umebaini kuwa zinawabeba zaidi wazawa kuliko wageni ili kuhamasisha Watanzania wengi kutembelea vivutio vya utalii wakati huu.
Tozo hizo ambazo hutozwa kwa viwango tofauti kulingana na hifadhi ambayo mtu anatembelea, wageni wanalipa zaidi ya robo tatu ya fedha anayotakiwa kulipa mtalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Leo tunakuletea tozo zinazotozwa katika baadhi ya Hifadhi za Taifa ambazo unaweza kuzitembelea mwaka 2020/21 kulingana na unene wa mfuko wako.
Tozo ya kiingilio humuwezesha mtalii kuingia hifadhini na kujionea vivutio mbalimbali wakiwemo wanyama kama tembo. Picha| Mama Africa Projects&Tours.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
Watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano wao hawatalipa fedha yoyote wakati wa kuingia katika hifadhi hiyo iliyopakana na hifadhi ya Ngorongoro ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 30,000.
Kwa Watanzania na wananchi wa EAC wenye miaka zaidi ya 16 watatozwa Sh10,000 na kwa wale wenye miaka mitano hadi 15 watatakiwa kulipa Sh2,000 kwa kila mtu.
Kwa mgeni aliye juu ya miaka 16 anayetoka nje ya EAC itabidi agharamie Dola za Marekani 60 ( Sh139,207) huku yule aliye na miaka kati ya 5 na 15 akitakiwa kugharamia Dola 20 (Sh46,406).
Watakaopata fursa ya kutembelea hifadhi hiyo, watajionea wanyama kama digidigi, swala na pundamilia ambao huipamba hifadhi hiyo kwa misimu tofauti tofauti ya mwaka huku baadhi yao wakikimbilia Ngorongoro kutafuta majani mwezi Januari.
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro
Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa hekari 75,575 inavutia watalii siyo tu kwa wanyama bali kwa mlima Kilimanjaro ambao ndiyo mlima mrefu zaidi barani Afrika.
Ili kuingia kwenye hifadhi hiyo, watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni bure huku wageni wanaotoka nje ya EAC wenye miaka mitano hadi 15 wakilipia dola 20 (Sh46,406) na waliozidi miaka 16 wakitakiwa kulipa dola 70 (Sh162,376).
Kwa wakazi wa EAC, wanatakiwa Sh10,000 na wenye miaka mitano hadi 15 atagharamia Sh2,000 tu.
Zinazohusiana:
- Saadani: Mahali unapoweza kuwaona simba, twiga wakila upepo wa ‘beach’
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii.
- Prince William atua Tanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wanyamapori
Hifadhi za Taifa za Arusha, Tarangire na Ziwa Manyara
Hifadhi hizi zinatozo gharama zinazofanana. Wakati Manyara ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 330, Tarangire imechukua kilometa za mraba 2,600 kwenye ardhi ya Tanzania na hifadhi ya Taifa ya Arusha ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 137.
Hifadhi hizi zinakupatia muda wa kustaajabu wanyama kama tembo, tumbili, sokwe na twiga.
Ikiwa ni bure kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, dola 45 (Sh104,392) zitamtoka mgeni mwenye umri zaidi ya miaka 16 huku yule mwenye umri wa miaka mitano hadi 15 akitozwa dola 15 sawa na Sh34,799.
Kwa wakazi wa EAC, Sh10,000 itahitajika kutoka kwa mtalii mwenye miaka 16 na zaidi huku Sh2,000 ikimtoka kijana mwenye miaka mitano hadi 15.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe
Hifadhi hii ndiyo hifadhi yenye viwango vya juu zaidi vya tozo kati ya hifadhi zote nchini, kwa watalii wanaotoka nje ya EAC ambapo mtalii mwenye miaka zaidi ya 16 atahitajika kulipa dola za Marekani 100 (Sh231,988) huku kijana mwenye miaka 5 hadi 15 akilipia dola 20 (Sh46,397).
Mtanzania na mkazi wa Afrika Mashariki mwenye miaka kati ya 5 na 15 atalipa Sh2,000 ikiwa ni pungufu ya mara tano ya mtalii mwenye umri zaidi ya miaka 16 ambaye anatakiwa kulipa Sh10,000.
Katika hifadhi ya Gombe, nyani aina ya sokwe ndiyo nyumbani. Picha|Gorrilla Trekking.
Hifadhi zingine
Kwa wakazi wa EAC wenye umri wa miaka zaidi ya 16 wanaotaka kwenda hifadhi za Mikumi, Ruaha, Rubondo, Saadani, Kitulo, Mkomazi, Milima ya Udzungwa, Katavi, Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe na Kisiwa cha Saanane, watalipa Sh5,000 huku wenye miaka kati ya 5 na 15 watalipa 2,000.
Wageni nje ya EAC wenye miaka zaidi ya 16 wao watalipa dola za Marekani 30 (Sh69,609) huku wenye umri wa miaka 5 hadi 15 watalipa dola 10 tu (Sh23,202).
Kwa watoto wote chini ya miaka mitano hawahitaji kulipia senti yoyote kuuona uzuri wa Tanzania.
Utaenda hifadhi gani kati ya hizo mwaka huu ili kujionea uzuri wa Tanzania?