November 24, 2024

Matokeo ya kidato cha sita 2020 sasa hadharani

Ufaulu waongezeka kidogo kwa asilimia 0.03

  • Necta yasema ufaulu wa madaraja ya I,II an III umeimarika. 
  • Wanafunzi watano wafutiwa matokeo kwa udanganyifu.

Dar es Salaam. Hatimaye Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita mwaka 2020 huku ufaulu wa jumla ukiongezeka kiduchu kwa pointi hadi kufikia asilimia 98.38 kutoka asilimia 98.32 iliyorekodiwa mwaka jana.  

Katibu Mtendaji wa Necta Dk Charles Msonde amewaambia wanahabari visiwani Zanzibar Ijumaa (Agosti 21 2020) kuwa wanafunzi 82,440 kati ya watahiniwa 84,212 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Ongezeko la ufaulu katika mwaka huu ni sawa na asilimia 0.03 kutoka kiwango cha ufaulu wa jumla cha mwaka 2019.

“Aidha, ubora wa ufaulu umezidi kuimarika kwa kuwa idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika madaraja ya I, II na III imeongezeka kwa asilimia 1.13 kutoka asilimia 96.61 na kuwa asilimia 97.74 mwaka 2020,” amesema Dk Msonde.

Katika matokeo hayo, wasichana waliopata ufaulu wa daraja la I hadi la III ni 31,786 sawa na asilimia 98.24 ya wasichana wote waliofanya mtihani huo kikiwa ni kiwango kikubwa kidogo kuliko wavulana kwa uwiano.

Wavulana 40,444 sawa na asilimia 97.35 walifaulu katika madaraja hayo ya juu, takriban asilimia moja nyuma ya wasichana.

Hata hivyo, baraza hilo limewafutia matokeo wanafunzi watano waliobanika kufanya udanganyifu katika mtihani huo uliofanyika kati ya Juni na Julai mwaka huu.

Tofauti na miaka iliyopita, wanafunzi wa kidato cha sita walifanya mitihani kipindi hicho badala ya Mei baada ya shule kufungwa kwa miezi mitatu ili kupunguza kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona (Covid-19).