November 24, 2024

Mjasiriamali abuni mzinga wa kufugia nyuki nyumbani

Unaweza kuwekwa katika bustani ya nyumbani kama pambo na kuzalisha asali ya nyuki wasio na madhara kwa binadamu.

  • Unaweza kuwekwa katika bustani ya nyumbani kuzalisha asali ya nyuki wasio na madhara kwa binadamu. 
  • Mizinga hiyo inatumika kama mapambo na kivutio kwa wageni wanaokuja nyumbani.
  • Ni njia ya kujipatia kipato na kuongeza uzalishaji wa asali. 

Mwanza. Sasa unaweza kuondoa kile ulichokuwa unakiamini kuwa mizinga ya nyuki ni lazima ikae porini. Unaweza kuwa na mzinga wako nyumbani na ukafuga nyuki kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo mapambo ya nyumbani. 

Ni ‘ubunifu’ ndiyo neno ninaloweza kulitumia baada ya kukutana na mjasiriamali ambaye amebuni mzinga wa nyuki ambao pamoja na kutumika kutengeneza asali lakini unaweza kutumika maeneo ya makazi ya watu.

Ni mjasiriamali Subya Katulanda  kutoka Wilaya ya Sengerema ambaye nimekutana naye katika maonyesho ya Nane Nane (Wakulima) yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza. 

“Kwa sasa nimejikita kwenye utengenezaji miziga ya kufugia nyuki hususan hawa wadogo ambao wanafugika hata maeneo ya nyumban,” anasema Katulanda ambaye amefanya kazi ya kutengeneza mizinga kwa miaka 20 hasa ya kufugia nyuki porini na biashara.

Mizinga ya kijana huyo unayoweza kuweka nyumbani kwako ni kwa ajili ya kufuga nyuki wadogo wasiokuwa na madhara kwa binadamu.

Aina hiyo ya ufugaji wa nyuki inafaa watu wenye bustani nyumbani ambapo wanaweza kupendesha mazingira ya nyumbani kwa kuwa na wadudu hao ambao wanatoa milio yenye utulivu na furaha. Anasema ana muda wa mwaka mmoja toka aanze ufugaji wa nyuki zoezi linaloenda sambamba na kupata elimu ya ufugaji.

Mjasiriamali huyo aliyeanza kazi hiyo mwaka mmoja uliopita, licha ya kuwa anatengeneza kwa ajili ya watu wengine, kwa sasa anamiliki mizinga 30 ambayo anatarajia kuvuna lita 70 za asali hadi ifikapo Disemba mwaka huu huku ndoto yake ni kutengeneza mizinga 500. 

Mzinga aliotengeneza Katulanda ambao una sehemu ya juu ya kupandia maua yanayohitajika n anyuki. Picha|Mariam John.

Alivyopata wazo la kutengeneza mizinga ya nyumbani

Fundi siku zote akili yake lazima aishughulishe kubuni vitu vipya vinavyolenga kuboresha maisha ya watu kwa kutumia teknolojia rahisi. Na hivyo ndivyo alivyofanya Katulanda.

“Baada ya kuona mizinga mingi inayotengenezwa inafugia nyuki porini nikaona kwanini tusitengeneze mizinga ambayo inaweza kufuga nyuki hata maeneo ya mijini? ndio nikapata wazo la kutengeneza mzinga huu,” anasema mjasiriamali huyo wakati akiongea na Nukta (www.nukta.co.tz).

Ili mzinga huo ambao unakuwa na ukubwa mita za mraba 50 ufanye kazi unatakiwa kutengenezewa bustani yenye mazingira ambayo ni kivutio cha  nyuki ikiwemo maua na miti. 

Kwa mujibu wa Katulanda, mzinga huo hauna tofauti na mingine kwani una sehemu mbili ya juu na chini. Sehemu ya chini ni ya malikia anapotaga mayai na kuzaa watoto. 

“Sehemu ya juu ni nyuki wengine wafanyakazi wanaopaki asali na katikati ya mzinga huo kuna kioo kinachomzuia malikia asipande juu,” anasema na kuongeza kuwa mzinga huo unaweza kumpatia mfugaji asali nzuri kwa matumizi mbalimbali. 


Soma zaidi: 


Kwa mfugaji anayependa kupata asali, chumba cha juu ndiyo huifadhi  masega ya asali halisia yasiyochanganywa na watoto wala mayai.

Anasema pia mzinga huo unapaa ambalo hupandwa maua yanayotumiwa na wadudu hao kutengeneza asali na kuwa kivutio kwa watu wanaokutembelea nyumbani. 


Soko la mizinga likoje

Katulanda anasema soko la mizinga hiyo lipo lakini mwitikio bado siyo mkubwa ikizingatia kuwa watu wengi wamezoea kufuga nyuki porini na siyo nyumbani.

Lakini anaendelea kutoa elimu kwa watu kuwashawishi kutumia teknolojia hiyo na kabla mteja hajachukua mzinga hupewa mafunzo maalum ili kumuweka salama na kuhakikisha wadudu hao wanamfaidisha. 

Mafunzo hayo yatamsaidia mfugaji kuepukana na changamoto zinazowakumba wafugaji wengine wa nyuki ikiwemo wanyama na wadudu kama sisimizi ambao ni maadui wa nyuki.

Baadhi ya watu wakiangalia mzinga aliotengeneza Katulanda katika maonyesho ya Nane Nane (Wakulima) yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza. Picha|Mariam John.

Serikali inavyowasaidia wajasiriamali

Afisa Mistu na Nyuki wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Deogratius Justus anasema wanashirikiana vizuri na wadau kuhakikisha wanatoa fursa kwa wabunifu kama Katulanda waweze kutambulika na kuwafikia watu wengi kwenye jamii. 

“Mpaka hapa tunaona sekta inakua na kwa upande wa uzalishaji na soko lenyewe ambapo hapo awali asali ilitumika kama sehemu ya kula kama utamu wake lakini kwa sasa wanaongeza thamani ya sekta hiyo,” anasema Justus.

Anasema wanaendelea kutoa elimu ili kuhamasisha wananchi waweze kufuga kisasa na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya asali ili kukuza vipato vyao vitakavyosaidia kuboresha maisha ya familia zao.