November 24, 2024

Senti zangu mbili kuhusu uzoefu wa maumivu

Ukipata maumivu ya kisaikolojia au kifisiolojia, muone daktari akusaidie.

  • Maumivu ni namna ya mwili kuwasilisha taarifa za hitilafu fulani katika mifumo yake.
  • Ukipata maumivu ya kisaikolojia au kifisiolojia, muone daktari akusaidie.

Umeamka asubuhi, una haraka hivi, umechelewa sana kazini au shuleni? Katika kujiandaa na pirika pirika za ndani ya nyumba mara unajikwaa kwa kidole chako cha mwisho. 

Kimsingi siku yako itakua imeanza vibaya maana maumivu yake siyo madogo yakichochewa na mgandamizo uliotokana na hatua zako za haraka. Siyo lengo langu tukae humu kwenye hizi hadithi za kujikwaa leo. Maumivu ni nini hasa? Kuna wakati maumivu ni mazuri kweli? Ni vipi kama tusingekua tunasikia maumivu?

Kitaalamu maumivu ni hali au hisia isiyopendeza ambayo huweza kuwa ya kawaida ama isiyovumilika kabisa.  Maumivu yanahusisha elementi za kisaikolojia na kifiziolojia vilevile. 

Sehemu ya kifisiolojia huhusisha Zaidi utambuzi wa kineva ambao hutokana na kusisimka kwa neva hizi za mwili. Maumivu yanaweza kuwa sehemu moja tu au yanaweza kuwa sehemu iliyosambaa, mfano miguu yote au hata mwili mzima. Maumivu haya hubebwa na neva maalumu hadi kwenye ubongo na huko hupata tafsiri kulingana na kiwango na ukubwa wa maumivu yenyewe. 

Unaposikia maumivu mwili wako unakupa taarifa ya kuwepo kwa hitilafu sehemu fulani kwenye mwili wako. Hali hii hukufanya kuchukua tahadhari kwamba mwili unahitaji huduma au una tatizo sehemu fulani. Kwa hiyo tunaweza kusema maumivu ni namna ya mawasiliano ya mwili bila shaka. 

Hata hivyo, kuna wakati maumivu haya hayahitaji msaada mkubwa wa kitabibu. Yaani ni aidha yanatokana na ukubwa wa shughuli uliyofanya, uchovu uliokithiri au pumziko la kutosha linaloweza kutosha kabisa kuondosha hali hiyo. Wakati mwingine ni sababu ya kuchanika kidogo kwa tishu ndogo baada ya mazoezi makali na kadhalika.

Ukipata maumivu yoyote usipouzie, hiyo ni namna ya mwili kukuambia una tatizo linalohitaji tiba. Picha| Patient Pleasers.

Kwa nini maumivu?

Ni wakati gani unapaswa kutilia maanani maumivu? Hili ndiyo suala kubwa na mzizi wa ninachokusudia kukuweka bayana leo. 

Changamoto kubwa ni namna watu tunapuuzia mawasiliano ambayo miili yetu hutupatia na mwisho wa siku hujikuta tukiwa na matatizo makubwa ambayo tungeyatilia maanani yangepata msaada wa kitabibu haraka na kupona kabisa.

Maumivu yaweza kuwa ya muda mfupi au maumivu sugu. Yanaweza kuwa ya kujirudia rudia au yanayotokea kwa kipindi kifupi kisha kupotea kabisa. 

Dawa za maumivu za baridi yaani ambazo unaweza kutumia bila maelezo ya daktari au cheti maalumu cha dawa hulenga kukupa ahueni ya maumivu kwa muda mfupi na kukuwezesha wewe kuendelea na shughuli zako. Lakini pindi maumivu hayo yanapozidi au yanapokuwa ya kujirudia mara kwa mara ni vyema sasa ufike hospitali na siyo kuongeza dozi nyigine ya dawa.


Zinazohusiana:


Madhara ya kupuuzia maumivu

Baadhi ya magonjwa kama saratani huanza kwa kuleta bugudha za kawaida kama hizo na watu wengi hupuuza na kutumia dawa za maumivu hadi pale hali inapokua mbaya zaidi. Na mwisho huwa wanakua wamechelewa sana na kujikuta na hali mbaya za kiafya. 

Maumivu yako ni sugu, yanajirudia rudia au ni makali na ya muda mfupi? Huna haja ya kupuuzia maumivu hayo. Fika hospitali upate uchunguzi wa kina wa tatizo lako na uhudumiwe ipasavyo. Mueleze daktari wako kuhusu maumivu hayo, eneo la maumivu na iwapo yamesambaa na kadhalika.

Maumivu pia yaweza kuwa ya kisaikolojia Zaidi. Yatokanayo na hisia fulani au msukumo. Pia yanaweza kuwa ya kufikirika kabisa yasiyotokana na eneo lolote kuwa na shida. 

Kuna aina ya maumivu ambayo huwakuta watu waliopata kukatwa sehemu za viungo vyao ambapo wao huhisi maumivu sehemu ambayo imekatwa ilhali haipo. Maumivu haya huitwa “Phantom Pain” na hutokana na ufahamu wao kuhisi kiungo kile bado kipo au bado ni sehemu ya mwili. 

Maumivu ya kisaikolojia huitaji msaada mkubwa wa kisaikolojia kwani huweza athiri namna mtu anavoingiliana na jamii, utendaji, uwezo wa kufanya kazi na hata mahusiano. Maumivu haya yanaweza kumpa mtu msongo na mkazo. 

Hivyo basi nakupa rai ufahamu ya kwamba maumivu ni namna ya mwili kuwasilisha taarifa za hitilafu fulani katika mifumo yake na hivyo ni vyema kutilia mkazo pale maumivu yanapokua makali na ya ghafla au yanayojirudia mara kwa mara. Punguza kabisa uraibu wa dawa za maumivu kwa tatizo moja. MUONE DAKTARI WAKO LEO.

NIP0!! 

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.